Maafa yafunga mwaka 2014, Basi laua wanne, 40 wajeruhiwa. Lori laparamia nguzo ya umeme, lalipuka na kuteketeza kwa moto maduka, nyumba

  Basi laua wanne, 40 wajeruhiwa. Lori laparamia nguzo ya umeme, lalipuka na kuteketeza kwa moto maduka, nyumba
Wananchi wakishuhusia moto ulisababishwa na lori la mafuta lililolipuka baada ya kugonga nguzo ya umeme na kuteketeza nyumba kadhaa, maduka, magari na pikipiki katika mji wa Handeni mkoani Tanga jana.
Siku  moja tu baada ya kutokea vifo na uharibifu mkubwa wa mali katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na mvua zinzoendelea kunyesha, majanga mengine yameendelea kutokea kuelekea mwishoni mwa mwaka huu wa 2014.
Vifo vya watu wasio na hatia vimetokea, watu kujeruhiwa na uharibifu mwingine mkubwa wa mali umetokea tena na kuacha vilio vingine.

Katika janga la kwanza, watu wanne  wamekufa  papo hapo na wengine 40 kujeruhiwa vibaya, baada ya mabasi mawili ya kubebea abiria kugongana uso kwa uso katika eneo la Uchira, nje kidogo ya Manispaa ya  Moshi, mkoani Kilimanjaro.

 Ajali hiyo imeyahusisha mabasi mawili Toyota Coaster, mali ya Kilenga Transport baada ya kugomngana na basi dogo ya Toyota Hiace lililokuwa likitokea wilayani Mwanga kuelekea mjini Moshi.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Godfrey Kamwela, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana alasiri na kusema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.

“Ni kweli ajali imetokea majira ya alasiri na uchunguzi  kuhusu chanzo cha ajali hiyo  unaendalea, lakini majeruhi wa ajali hiyo  wamekimbizwa katika Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu,” alisema Kamwela.

Shuhuda wa ajali hiyo, Daud Kileo, alisema Coaster lilikuwa likitoka mjini Moshi kuelekea Same wakati Hiace lilikuwa likitokea Mwanga kuelekea Moshi mjini.

“Ajali ilitokea baada ya gurudumu la Coaster kupasuka  na kwenda kuvaana na Hiace  iliyokuwa ikitoka Mwanga,” alisema Kileo.

 Shuhuda mwingine, Eva Mushi, alisema magari yalikuwa katika mwendo kasi na kulilaumu Jeshi la Polisi kwa askari wake kushindwa kufika eneo la tukio mapema.

“Inasikitisha kuona  polisi wetu wa usalama barabarani hawapo makini katika ukaguzi wa mwendo kasi wa magari ya abiria hasa kipindi hiki cha sikukuu, hali ambayo inasababisha watu wengi kutomaliza mwaka kwa usalama kutokana na madereva kuwa na taama ya kufanya biashara,” alisema.

Ofisa Habari wa KCMC, Gabriel Chiseo, alithibitisha  kupokea watu atano wakiwa mahututi na kuingizwa katika chumba cha uangaliza maalumu (ICU).

LORI LALIPUKA, LATEKETEZA NYUMBA, MAGARI
Katika tukio la janga la pili, nyumba sita za makazi ya watu, vyumba 16 vya biashara, magari matatu  na pikipiki moja Vimeteketea kwa moto na watu watatu kujeruhiwa baada ya gari lililosheheni mafuta ya Petroli  kulipuka kisha kugonga nguzo za umeme wilayani Handeni Mkoa wa  Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, akizungumza katika mahojiano na NIPASHE , alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:25 asubuhi katika Mtaa wa Kativeta Kata ya Chanika mjini Handeni.

Muhingo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, alisema majeruhi hao walipelekwa  Hospitali ya Wilaya ya Handeni kwa matibabu.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni  pamoja na dereva wa gari la kikosi cha zima moto ambaye alirukiwa na vioo vya gari baada ya wananchi kulipiga mawe kutokana na kuchelewa kufika eneo la tukio.

Gari hilo lilichelewa kufika eneo la tukio kwa sababu lilitokea wilayani Korogwe kutoka na wilaya ya Handeni kukosa gari.

 “Kutokea kwa ajali hii kumetoa fundisho kubwa kwa mji mkubwa kama huu wa Handeni kukosa gari la zima moto ni janga, sasa hasira ya wananchi yote ilikuwa ni hiyo kwa nini halmashauri ikose gari maana gari lililokuwa likitumika ni lile la kuvuta maji machafu na kutupa nje, ” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai, alisema ajali hiyo iliyohusisha lori aina ya Scania mali ya Said Khalfan, mkazi wa wilayani Handeni ilitokea baada ya kupoteza mwelekeo  kisha kugonga nguzo ya umeme iliyokuwa nje ya nyumba na hatimaye kulipuka.

Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa Mohamed Athman (20) ambaye ni utingo wa lori hilo,  mkazi wa Kivesa, dereva wa lori hilo,  Alli Said (50),  mkazi wa Chogo na Zuberi Salehe (24) muuza mafuta katika kituo cha kuuza mafuta cha mjini Handeni.

Kashai alisema kati ya majeruhi hao, Athman hali yake ni mbaya na taratibu za kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga kwa matibabu zaidi zimefanyika.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni baada ya dereva wa lori hilo kujaribu kumkwepa mwendesha pikipiki maarufu kama boda boda na kusababisha gari kupoteza mwelekeo na kugonga ukuta wa nyumba ambao ulikuwa usawa wa nguzo ya umeme na  kulipuka moto.

Alisema wakati tukio hilo likitokea kulikuwa na gari aina ya Toyota Canter mali ya John Shayo, pikipiki  ambavyo viliteketea kwa moto.

 Kashai alisema baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo la tukio walilishambulia kwa mawe gari la Kikosi cha Zima Moto mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na kuliharibu kutokana na kuchelewa kufika eneo la tukio.

Alisema wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kuharibu gari hilo wanasakwa na polisi.

“Gari limetoka umbali wa zaidi ya kilometa 70 kutoka Korogwe kuja Handeni kuwasaidia wanafika mnawazuia kufanya kazi yao nini maana yake ni uvunjifu wa sheria lakini kwa ubinadamu si sahihi walikuja kwa nia njema sana, “alisema Kashai.

Kufuatia tukio hilo, kulizuka tafrani kubwa ya wananchi ambao nyumba zao zimetekea kwa moto kwa kupandwa na hasira kutokana na gari la zima moto kuchelewa kufika hali iliyowafanya kulizuia  kufanya kazi yake huku wakirusha mawe.

Gari hilo  lilifika  eneo la tukio baada ya saa moja na  wananchi kuanza kulishambulia kwa mawe na kulizuia lisifanye kazi.

“Hatutaki tokeni mlikuwa wapi muda wote mpaka nyumba zimeteketea toeni uzushi wenu hapa usanii tu tumechoka tokeni wauaji wakubwa,” walisikika wakisema baadhi ya wananchi hao.

Katika tukio hilo,  vibaka nao walitumia mwanya wa uokoaji kwa kujinufaisha kwa kuiba baadhi ya vitu vilivyokuwa vikitolewa nje ya maduka hayo na kukimbia.

Mmoja wa wananchi waliokuwepo eneo la tukio, Suleiman Iddi,  alisema ajali hiyo imegusa hisia za wakazi wa Handeni hasa kwa kuzingatia kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao wanafanya shughuli zao kwa mikopo na kwamba hali hiyo imewaweka pabaya kiuchumi.

“Januari hii inafika watoto wanataka kwenda shule halafu kitega uchumi kinateketea kweli ni jambo la huzuni sana hali ya maisha kwa sasa ni ngumu mno imetusikitisha sana”,alisema iddi.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم