Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad amesema atapambana katika vikao na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein iwapo baadhi ya wananchi wataendelea kunyimwa shahada za
wapigakura kwa kisingizio cha ukaazi.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana alipohutubia
mkutano wa hadhara wa CUF uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wake, Profesa
Ibrahim Lipumba katika Uwanja wa Jarida, Wete Pemba.
Alisema kuna viongozi wa Serikali za Mitaa
(masheha) kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa ambao wameanza
kupanga mikakati ya kutaka kuwanyima shahada za wapigakura baadhi ya
wananchi kwa madhumuni ya kuibeba CCM katika uchaguzi mkuu.
“Masheha eleweni nazungumza kama makamu wa kwanza
wa rais, suala la ukiritimba sasa basi na kama hamtaki sisi tutapambana
na Dk Shein katika vikao yeye, ndiye anayewateua,” alisema Maalim Seif.
Kwa miaka mingi yamekuwapo malalamiko kutoka CUF
kwamba masheha wamekuwa wakiwanyima vitambulisho vya upigaji kura baadhi
ya Wazanzibari, wakisema si wakaazi wa Zanzibar.
Akishangiliwa na wafuasi wa CUF, Maalim Seif
alisema kama mipango itakwenda kama ilivyopangwa, hakuna wa kuizuia CUF
kuingia Ikulu, hivyo akawataka wana-CUF kuendeleza umoja na mshikamano
kabla ya uchaguzi huo.
Alisema umoja ni nguvu na ndiyo maana Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), umefanikiwa kuandika historia mpya katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya kupata matokeo ya kuridhisha.
Mwanasiasa huyo alisema madhara ya kukataa umoja
ndiyo yaliyoiathiri Zanzibar katika Bunge la Katiba baada ya wajumbe
wake kutetea masilahi ya chama badala ya nchi.
Akihutubia mkutano huo, waziri wa zamani wa SMZ,
Mansoor Yusuph Himid alisema njia ya Maalim Seif kuingia Ikulu mwakani
ni nyeupe.
Alisema CUF kipo imara na kwamba jambo muhimu ni
wanachama na wafuasi wake kuendeleza umoja na mshikamano kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi huo.
“Njia ya kuingia Ikulu nyeupe, muhimu tukaze buti kufikia malengo ya kuleta mabadiliko ya kweli,” alisema Mansoor.
Profesa Lipumba alisema suala la Katiba ndiyo
limeimaliza CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na
wananchi wengi kupinga kitendo cha rasimu ya Jaji Warioba kubadilishwa
na kuondoa vifungu muhimu vilivyokuwa vikiwabana mafisadi na viongozi
wasiokuwa waadilifu.
Post a Comment