Maalim Seif kumvaa Dk Shein kuhusu ukaazi

Zanzibar. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema atapambana katika vikao na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein iwapo baadhi ya wananchi wataendelea kunyimwa shahada za wapigakura kwa kisingizio cha ukaazi.
Maalim Seif alitoa msimamo huo jana alipohutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba katika Uwanja wa Jarida, Wete Pemba.
Alisema kuna viongozi wa Serikali za Mitaa (masheha) kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya na mikoa ambao wameanza kupanga mikakati ya kutaka kuwanyima shahada za wapigakura baadhi ya wananchi kwa madhumuni ya kuibeba CCM katika uchaguzi mkuu.
“Masheha eleweni nazungumza kama makamu wa kwanza wa rais, suala la ukiritimba sasa basi na kama hamtaki sisi tutapambana na Dk Shein katika vikao yeye, ndiye anayewateua,” alisema Maalim Seif.
Kwa miaka mingi yamekuwapo malalamiko kutoka CUF kwamba masheha wamekuwa wakiwanyima vitambulisho vya upigaji kura baadhi ya Wazanzibari, wakisema si wakaazi wa Zanzibar.
Akishangiliwa na wafuasi wa CUF, Maalim Seif alisema kama mipango itakwenda kama ilivyopangwa, hakuna wa kuizuia CUF kuingia Ikulu, hivyo akawataka wana-CUF kuendeleza umoja na mshikamano kabla ya uchaguzi huo.
Alisema umoja ni nguvu na ndiyo maana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umefanikiwa kuandika historia mpya katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya kupata matokeo ya kuridhisha.
Mwanasiasa huyo alisema madhara ya kukataa umoja ndiyo yaliyoiathiri Zanzibar katika Bunge la Katiba baada ya wajumbe wake kutetea masilahi ya chama badala ya nchi.
Akihutubia mkutano huo, waziri wa zamani wa SMZ, Mansoor Yusuph Himid alisema njia ya Maalim Seif kuingia Ikulu mwakani ni nyeupe.
Alisema CUF kipo imara na kwamba jambo muhimu ni wanachama na wafuasi wake kuendeleza umoja na mshikamano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
“Njia ya kuingia Ikulu nyeupe, muhimu tukaze buti kufikia malengo ya kuleta mabadiliko ya kweli,” alisema Mansoor.
Profesa Lipumba alisema suala la Katiba ndiyo limeimaliza CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kutokana na wananchi wengi kupinga kitendo cha rasimu ya Jaji Warioba kubadilishwa na kuondoa vifungu muhimu vilivyokuwa vikiwabana mafisadi na viongozi wasiokuwa waadilifu.

Post a Comment

أحدث أقدم