
Katuni.
Lawama za kipindi cha uhamisho kuja mapema mno baada ya mechi saba tu za ligi hiyo zinazipitia kando klabu, lakini haziwezi kuepuka lawama ya kusajili kwa ajili ya kufurahisha mashabiki.
Imeshuhudiwa klabu ya Simba ikimuacha mshindi wa tuzo ya 'kiatu cha dhahabu' cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania msimu uliopita baada ya kufunga goli moja tu katika mechi saba hadi sasa msimu huu.
Kwa namna yoyote, kitendo cha kumuacha mfungaji bora baada ya mechi saba ni lazima kitazua maswali.
Na kauli za kocha wa Simba, Patrick Phiri kwamba mchezaji huyo ni jembe, zinatia shaka kama ni kweli mwalimu ndiye aliyeidhinisha kuachwa kwa Mrundi huyo aliyetokea katika klabu ya Vital'O ya Burundi ambako nako alikuwa mfungaji bora wa ligi kuu na pia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
Zinaendeleza mitazamo kwamba makocha wa klabu zetu hawana kauli katika suala la mchezaji gani anunuliwe na yupi aachwe, mambo ambayo hakika yametufikisha hapa tulipo. Mahala pa kutolewa mapema katika michuano mikubwa. Mahala ambako neno ushindani katika michuano mikubwa halipo kwa vile daima tunakwenda kushiriki na si kushindana.
Usajili daima unapaswa kufanywa na kocha kwa sababu ndiye anayejua ni mbinu gani anahitaji kuzitumia na ni mchezaji wa aina gani anaweza 'kufiti' katika mfumo wake.
Ni kwa namna hiyo ndivyo ambavyo uwajibikaji wa kocha unaweza kupimwa.
Kusajili wachezaji kwa ajili ya kufurahisha mashabiki kuna madhara makubwa kwa timu yenyewe na kwa taifa pia.
Timu za Tanzania zimekuwa zikishindwa kung'aa katika michuano mikubwa ya Afrika licha ya mara kadhaa kutumia pesa nyingi katika kuzijenga.
Wafadhili na viongozi kuamua kusajili wachezaji wanaopendwa na mashabiki kwa kudhani kwamba ndiyo itakuwa salama ya kubaki madarakani ama kuendelea kujikubalisha kwa mashabiki, hakuwezi kututoa hapa tulipo.
Viongozi wa soka letu wanatakiwa wabadilike sasa. Waachie jukumu la kusajili kwa benchi la ufundi.
Na benchi la ufundi linapaswa kutambua kwamba linasajili kwa nia ya kusaka mafanikio ya Afrika.
Ni kwa malengo makubwa ndiyo unaweza kufanya maajabu kwa sababu miujiza katika soka haiji kwa kulala, bali kwa kufanya kazi ya ziada. Na kazi hiyo ya ziada inaanzia katika kujenga kikosi cha ushindani katika usajili.
Usajili ambao utalenga kupambana na TP Mazembe, kwa mfano, ndiyo ambao unaweza kufungua njia ya soka letu kutoka hapa lilipo pa kupania kushindana wenyewe kwa wenyewe tu.
Kujiwekea malengo makubwa kutasaidia kuinua soka la Tanzania kwani pale malengo makubwa yanapokwamia njiani kuelekea juu ndivyo yanavyozidi kuwapa hamasa ya kufika mbali zaidi mwakani.
Lakini usajili wa kulenga kuifunga Simba tu, au Yanga tu hauwezi kulifanya soka la nchi hii lipige hatua hata moja mbele ya hapa. Nchi itazidi kubaki nyuma kwa sababu mataifa mengine ambayo mpira wake ulikuwa chini kama Sudan na Ethiopia yatazidi kutupita tukiwa tumesimama.
Kwa kuwa klabu za Tanzania kwa muda mrefu sasa zimeonekana ni wasindikizaji katika michuano ya kimataifa, ilipaswa vipindi kama kilichomalizika cha usajili kutumika kimalengo.
Viongozi kukubali mgawanyo wa madaraka. Kwamba kama wameliamini benchi la ufundi na kulipa timu katika kusaka ubingwa wa nchi, wanapaswa pia kuwaamini katika kusaka aina ya wachezaji ambao watawasaidia kufanya ndoto zao kuwa kweli.
Kuendelea kumchagulia kocha wachezaji wa kucheza, kusajili wachezaji ambao hawamo kwenye mipango ya kocha ni kati ya mambo yatakayolifanya soka la Tanzania lisisogee kutoka hapa lilipo.
Kokote duniani kuna timu kubwa na ndogo, ndiyo. Lakini kwa malengo ya kufika mbali, daima watawala wapya katika kila jambo huibuka na Tanzania inaweza kuwa mtawala wa baadaye.
Tunahitaji kuona kama mabadiliko yaliyofanyika katika dirisha dogo la usajili yalilenga ushindani si kufurahisha mashabiki.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق