Maaskofu wazidi kuikaba koo Serikali

Dar/Zanzibar. Viongozi wa dini wamezidi kuikaba koo Serikali kuhusu kashfa ya Escrow na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Wakitoa mahubiri katika ibada takatifu ya sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo juzi, viongozi hao wamewataka viongozi wa Serikali kuwasaidia wananchi wao.

Askofu Augustine Shao wa Kanisa la Romani Katoriki Jimbo la Zanzibar  alisema  zoezi la kura ya maoni ya kupitisha Katiba mpya lisitishwe hadi wananchi watakapopewa elimu ya uraia ya kutosha kabla ya kufanyika mwakani.

kipindi cha miezi minne iliyobakia kabla ya wananchi kupiga Kura ya maoni akitoshi kutoa elimu ya uraia hasa kwa kuzingatia asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini kusikokuwa na huduma ya umeme na wengi wao wakiwa hawana nakala za Katiba inayopendekezwa tangu kupitishwa na Bunge la Katiba Oktoba mwaka huu.Askofu Shao alisema  mwakani ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu pia wahusika walitakiwa kuangalia hilo, lakini alisema iwapo wananchi watapatiwa elimu ya kutosha wanaweza kufanya uamuzi wa msingi na kufanikisha kupata Katiba yenye masilahi kwa taifa na wananchi wake.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la TAG Zanzibar,  Dickson Donald alisema kwamba Watanzania watapata Katiba bora kama watapewa elimu ya uraia ya kutosha na zoezi lenyewe kufanyika kwa uwazi bila ya mizengwe.

Alisema  wakati huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu mwakani ni vizuri Watanzania kuchagua viongozi kwa kuwapima uadilifu na uwezo badala ya kuangalia vyama na itikadi. Alisema kuwa vigezo hivyo iwapo vitazingatiwa Taifa litapata viongozi bora na kufanikiwa kudhibiti vitendo vya ufisadi na ubadhirifu na kuimarisha misingi ya utawala na sheria.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe alisema CCM imeshikwa na hofu kuwa upinzani unaweza kushika dola kupitia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. Askofu Kakobe alisema hofu hiyo ndiyo inayokifanya chama hicho tawala kuikumbatia Tume ya Uchaguzi isiyokuwa huru na haki, kushindwa kuboresha daftari la wapigakura na kupanga chaguzi zifanyike siku za Jumapili.

Katika hatua nyingine, aliwashangaa Ukawa kukubaliana kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao angali kuna tume isiyokuwa huru.

Aliongeza akisema Tume ya Uchaguzi iliyopo kwa sasa bado ni kiini macho kutokana na viongozi wake kuteuliwa na mwenyekiti wa CCM.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم