MAONI: Kashfa hizi kwa Serikali sasa basi

Jana katika tovuti hii tulitoa habari iliyowakariri viongozi wa dini wakionyesha kukerwa na vitendo vya ufisadi, wizi, uzembe ikiwamo kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi hao waliokuwa wakitoa mahubiri yao katika ibada ya Sikukuu ya Krismasi walisema ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, kukosa uhakika wa huduma bora za matibabu na elimu ni moja ya matatizo makubwa ambayo hivi sasa yanalisumbua taifa.
Walisema mbali na maisha ya ufukara na ukosefu wa huduma, sakata la escrow na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliyotolewa Jumatatu vimezidi kuzidisha hofu kwa Watanzania na kuwafanya waonekane kama hawana matumaini.
Walisema watu wengi wanaishi katika ulimwengu wa hofu kutokana na ufukara, ukosefu wa huduma, na kwamba  watu wanajiuliza watawasomeshaje watoto wao na watapata wapi huduma bora za matibabu.
Walienda mbali zaidi ya kueleza kuwa  fedha zilizochotwa katika akaunti ya escrow ni mali ya umma, kutokana na taarifa iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa ujumla ni kwamba ujumbe wa viongozi wa dini ulikuwa unatoa somo kwa Serikali kwamba sasa inapaswa kuzuia matendo haya maovu.
Pia, ujumbe huo ulikuwa unawakumbusha viongozi wa Serikali wajibu wao wa kuwapatia maisha bora wananchi.
Wananchi wanashangaa kuona wakati wao wanaishi katika maisha magumu, lakini baadhi ya viongozi wakionekana wakihusishwa kuchota mamilioni ya fedha za umma bila ya kuchukuliwa hatua stahiki.
Zipo kashfa nyingi ambazo zimetokea hapa nchini mpaka sasa, lakini kwa sababu hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa na zingine zinaendelea kuibuka kila siku.
Katika utawala wa awamu ya nne ambao ndiyo unaonekana kukumbwa na kashfa nyingi zaidi, ilianza na Kashfa ya Richmond, kashfa ya wizi Katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), Operesheni Tokomeza na sasa escrow.
Pamoja na kwamba kashfa hizi ziliitikisa Serikali kwa kila moja kwa wakati wake, kwa Richmond aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine walilazimika kujiuzulu na kashfa ya Epa walioiba walipewa muda wa kuzirejesha na kwa walioshindwa walifikishwa mahakamani.
Kashfa ya Operesheni Tokomeza iliwang’oa mawaziri wanne na kashfa ya escrow tayari imewang’oa vigogo wawili, mmoja kasimamishwa kazi na mwingine kawekwa kiporo.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم