Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa,Jacob Mwaruanda.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, mama aliyefanya ukatili huo (jina linahifadhiwa) ni mkazi wa mtaa wa Eden, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani hapa.
Inadaiwa mama huyo alifanya kitendo hicho baada ya kukasirishwa na kitendo cha mwanae huyo kupakua maharage kutoka kwenye chungu na kuyala.
Ilielezwa kuwa mama huyo alikuwa ameyapika maharage hayo kwa ajili ya mlo wa mchana.
Kamanda Mwaruanda alisema mama huyo alikamatwa na polisi Desemba 13, mwaka huu, saa tisa mchana kufuatia taarifa za siri kutoka kwa raia wema kwamba alikuwa akimnyanyasa mwanae huyo ambaye anasoma chekechea mjini hapa .
“Kufuatia taarifa hizo za siri askari polisi walifika nyumba kwa mtuhumiwa huyo saa tisa mchana na kumkuta mtoto huyo akiwa amefungiwa ndani akiugulia maumivu makali mikononi mwake baada ya kujeruhiwa vibaya na kuchomwa moto na mama yake mzazi” alisema.
Kwa mujibu wa mtoto huyo, alifanyiwa kitendo hicho baada ya kurejea nyumbani akitokea shule akiwa na njaa kali kwa kuwa tangu asubuhi alikuwa hajala chochote siku hiyo.
“Mie nasoma chekechea njaa ilikuwa imenibana, nilikuwa sijala chochote tangu asubuhi, hivyo niliamua kupakua maharagwe yaliyokuwa ndani ya chungu ambayo yalikuwa yamepikwa na mama yangu, mama alirejea nyumbani na kunikuta nikila maharage hayo alikasirika na akachukua fimbo na kuanza kunicharaza.”
“Nililia sana kwa maumivu lakini mama hakunihurumia, alichukua kamba akanifunga mikono yangu kisha akachukua kijinga cha moto akaanza kuniuunguza viganja, nilihisi maumivu makali sana,” alisema mtoto huyo huku akitokwa machozi.
Alisema baada ya kufanyiwa ukatili huo, bila matibabu yoyote wala chakula, akimkataza kutoka nje kwa siku nne hadi alipookolewa na askari polisi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Kamanda Mwaruanda alisema mama huyo atafikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment