Mtoto afanyiwa unyama na mama yake mzazi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa,Jacob Mwaruanda.
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita amefanyiwa visa vya kinyama na mama yake mzazi, ambaye  anadaiwa kumjeruhi vibaya kwa kumchoma moto mikono yake na kisha kumfungia ndani kwa siku nne akiugulia majeraha bila kutibiwa wala kula chakula.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda,  mama aliyefanya ukatili huo (jina linahifadhiwa) ni mkazi wa mtaa wa Eden, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani hapa.

Inadaiwa mama huyo alifanya kitendo hicho baada ya kukasirishwa  na kitendo cha mwanae huyo kupakua maharage  kutoka kwenye chungu na kuyala.
Ilielezwa kuwa mama huyo alikuwa ameyapika maharage hayo kwa ajili ya mlo wa mchana.

Kamanda Mwaruanda alisema mama huyo alikamatwa na polisi Desemba 13, mwaka huu, saa tisa mchana kufuatia taarifa za siri  kutoka kwa raia wema kwamba alikuwa akimnyanyasa mwanae huyo ambaye anasoma chekechea mjini hapa .

“Kufuatia taarifa hizo za siri  askari polisi walifika  nyumba kwa mtuhumiwa huyo saa tisa mchana na kumkuta mtoto huyo akiwa amefungiwa ndani  akiugulia maumivu makali  mikononi  mwake baada ya  kujeruhiwa vibaya na kuchomwa moto  na  mama yake mzazi” alisema.

Kwa mujibu wa mtoto huyo, alifanyiwa kitendo hicho baada ya kurejea  nyumbani akitokea shule akiwa na njaa kali kwa kuwa tangu asubuhi alikuwa hajala chochote siku hiyo.

“Mie nasoma chekechea njaa ilikuwa imenibana, nilikuwa sijala chochote tangu asubuhi, hivyo niliamua kupakua maharagwe yaliyokuwa ndani ya chungu ambayo yalikuwa yamepikwa na mama yangu, mama alirejea  nyumbani  na kunikuta nikila maharage hayo alikasirika na akachukua fimbo  na kuanza kunicharaza.”

“Nililia sana kwa maumivu lakini mama  hakunihurumia, alichukua kamba  akanifunga mikono yangu kisha akachukua kijinga cha moto akaanza  kuniuunguza  viganja, nilihisi maumivu makali sana,” alisema mtoto huyo huku akitokwa machozi.

Alisema baada ya kufanyiwa ukatili huo, bila matibabu yoyote wala chakula, akimkataza  kutoka  nje kwa siku nne  hadi alipookolewa na askari polisi na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.

Kamanda Mwaruanda alisema mama huyo atafikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم