Tibaijuka: Mimi, Prof Muhongo hatung`oki

  Atamba Kikwete anawategemea
  Afurahia mgao wa mabilioni Escrow
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akielezea msimamo wake wa kutojiuzulu katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.PICHA: KHALFAN SAID.
Siku mbili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kujiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, ameibuka na kusema yeye pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, hawawezi kuchukua uamuzi huo kwa sababu Rais Jakaya Kikwete anawategemea kwa uchapaji kazi wao.
Prof. Tibaijuka na Prof. Muhongo, ni miongoni mwa watuhumiwa wa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi; Jaji Werema; Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge; Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa na Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja.

Prof. Tibaijuka alitoa msimamo huo alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa ghafla jijini Dar es Salaam jana.

Alisema yeye na Prof. Muhongo wanafanya kazi kubwa, ambayo inamfanya Rais Kikwete awategemee na kwamba, wanafahamiana walipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
“Kazi za Muhongo alizopewa na Rais Kikwete zinaonekana kwa macho, kama nguzo za umeme, wananchi wanaona. Lakini kazi zangu hazionekani. Ni kama figo zilizoko ndani ya mwili wa binadamu. Kazi ya Wizara ya Ardhi ni kubwa kuliko watu wanavyofikiri,” alisema Prof. Tibaijuka.

Akijibu swali kama yeye ni kibaraka wa Prof. Muhongo kutokana na kupata mgawo katika fedha hizo, alisema yeye (Prof. Tibaijuka) hawezi kuwa kibaraka na hawezi kufanya kazi ya udalali.

Alisema yeye na Prof. Muhongo wanafahamiana na kwamba, hata Rais Kikwete anafahamu urafiki wao na hawawezi kuacha kushirikiana kwa sababu wote wamepewa kazi na Rais, ambaye atashangaa kusikia hawaongei.

Prof. Tibaijuka, ambaye alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 katika fedha hizo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing LTD, James Rugemalira, alisema kamwe hawezi kujiuzulu na pia anajivunia na kuona fahari kupata fedha hizo. Kampuni hiyo ya Rugemalira ilikuwa mwana hisa katika IPTL.

Alisema ni bora alivyopata fedha hizo na kuzipeleka katika shule yake kwa ajili ya kusaidia shughuli za elimu kwa watoto wa kike wasio na uwezo.

Kutokana na hali hiyo, alisema anahitaji kusifiwa kwa ujasiri wake wa kukiri kupokea fedha hizo na kuzitolea maelezo, ingawa alikosa nafasi hiyo katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).

Akijibu swali sababu za kutokutoa maelezo hayo mbele ya PAC, Prof. Tibaijuka alisema anayepaswa kuulizwa swali hilo ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Zitto Kabwe.Alisema PAC haikumwita ili atoe maelezo hayo, badala yake Bunge liliishia kutoa maazimio, ambayo mawili kati yake, moja likitaka wachunguzwe na lingine wawajibishwe.Prof. Tibaijuka alisema wakati azimio la kutaka wachunguzwe halijatekelezwa, azimio la kutaka wawajibishwe tayari linatoa hukumu dhidi yao.

Akijibu swali sababu za kugoma kujiuzulu, alisema fedha hizo hazijathibitishwa kuwa ni haramu.Alisema atajiuzulu tu iwapo itathibitika fedha hizo za Rugemalira, siyo halali.

Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo hazijathibitishwa na serikali kuwa siyo halali, kiasi cha yeye kutakiwa kujiuzulu nafasi yake serikalini.Alisema fedha hizo hazina uhusiano kati yake na nafasi ya uwaziri aliyonayo, kwani zilikwenda moja kwa moja kusaidia kulipa deni la Sh. bilioni mbili, ambazo moja ya shule zake ilikopo kutoka Benki M.

Prof. Tibaijuka alisema iwapo itabainika fedha hizo si halali atakuwa tayari kuzirudisha.“Iwapo fedha hizo zitathibitika siyo halali, Joha Trust itazirudisha, kama taasisi inavyoitwa nia njema, sisi hatuhifadhi fedha zisizo halali,” alisema Prof. Tibaijuka.

Alisema fedha hizo alizipokea Februari 12, mwaka huu, zilitokana na maombi ya awali kutafuta michango kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na wafadhili wa nje.Alisema hoja kwamba, alipokea mchango mkubwa, haina uzito kutokana aina ya mtu, ambaye alimpa mchango huo na kusema ni mtu mwenye fedha na pia ni mfanyabiashara.

“Labda mnafikiri unapoomba fedha kwa mtu kama Bill Gates unategemea atakuchangia kama kiasi gani? Siyo senti. Hata mimi nilipoambiwa na Rugemalira nikaangalie akaunti yangu ina shilingi ngapi na kukuta fedha nyingi, nilijua leo nimeamkia mkono wa kulia. Nilifurahi,”  alisema Prof. Tibaijuka.

Alisema fedha hizo alichangiwa kwa ajili ya kulipa sehemu ya deni la Sh. bilioni mbili anazodaiwa na Benki M.Prof. Tibaijuka alisema fedha hizo walikopa kwa ajili ya ujenzi wa bweni la shule lenye uwezo wa vitanda 163.

Alisema fedha hizo zimechangia maendeleo ya elimu kwa kuwatengenezea watoto mazingira bora.“Hii kitu inabidi tuwe makini kama Taifa, kwani mimi nilikuwa mtumishi Umoja wa Mataifa. Lakini sikuweza kubeba fedha. Na kuna mapesa kule. Iwe katika nchi hii, ambayo nafahamu hata wapigakura wangu wa kule Muleba Kusini na wakulima wanaishi maisha ya chini?” alihoji Prof. Tibaijuka.

Alisema uamuzi wa kuzitoa fedha hizo haraka katika Benki ya Mkombozi, ulifikiwa na Bodi ya Wadhamini ya Joha Trust, ambayo ilitoa maamuzi kwamba, zitumike kulipa deni la Benki M.Hata  hivyo, katika mkutano huo  Prof. Tibaijuka hakutoa nyaraka zozote zikiwamo risiti zinazoonyesha deni hilo lilivyolipwa kupitia benki hiyo.
Alisema analazimika kutoa maelezo hayo katika vyombo vya habari kutokana na kutopewa nafasi ya kufanya hivyo mbele ya PAC.

“Kitendo cha mimi kuitwa Escrow, kwa kweli si kizuri na kinashusha maadili hata ya wewe unayekifanya. Waandishi msiandike, ambacho kinasemwa. Fuatilieni kwa umakini. Kwanza hii inaweza kuliweka Taifa katika image (taswira) mbaya. Nilitumikia Umoja wa Mataifa (UN), hata Katibu Mkuu wa UN akiona nimechukua fedha hizi hii, haipendezi,” alisema Prof. Tibaijuka.

Alisema serikali bado haijathibitisha kuwa fedha za Rugemalira ni haramu kiasi cha yeye kulaumiwa.Kutokana na hali hiyo, alionya kuwa kujiuzulu kusiwe kama mtindo, kwani fedha hizo hazikugusa utendaji kazi wake kama mtumishi wa serikali.Alisema mitandao inaendelea kuandika na asilimia kubwa wakimtukana.

Matamshi hayo yametolewa na Prof. Tibaijuka katika kipindi, ambacho Rais Kikwete akitarajiwa kutoa maamuzi kuhusiana na kashfa hiyo wakati wowote.Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es Salaam, Jumapili ya wiki iliyopita, Rais Kikwete anatarajiwa kutoa maamuzi hayo ndani ya wiki hii.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم