Dar es Salaam.Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa
amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa Jumuiya
ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
Ni baada ya wakili wa washtakiwa hao wa ugaidi,
Abubakar Salim kumtaka ajitoe kuisikiliza kesi hiyo ili iweze kupangiwa
hakimu mwingine ambaye atatoa uamuzi juu ya hoja zao walizozitoa
mahakamani hapo Septemba 19,2014.
Salim aliiambia mahakama kuwa baada ya kushauriana
na wateja wao na uamuzi uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Dk Fauzi
Twaib wakaona kuwa ni ukweli kuwa Hakimu Liwa alikwisha toa uamuzi wake
juu ya hoja zao Oktoba Mosi, 2014 kuwa mahakama hiyo ya kisutu haina
mamlaka ya kuzikiliza.
Alidai Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa
na Jaji Twaib umeelekeza kuwa Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya
kuzisikiliza hoja za washtakiwa hao wa ugaidi na hata kuzitolea uamuzi.
“Mahakama Kuu imeelekeza mawakili wa upande wa
utetezi kama tutakuwa na hoja mpya ama za zile za awali tuzitoe kwenye
mahakama hii ya Kisutu ili ziweze kutolewa maamuzi hivyo naona ni bora
ujitoe tupate neno kutoka kwa hakimu mwingine.”Alisisitiza kusema
wakili huyo mahakamani hapo.
Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola alimuomba
Hakimu Liwa asijitoe katika kuisikiliza kesi kwa madai sababu
zilizotolewa na upande wa utetezi za kumtaka ajitoe hazina msingi.
Kongola alieleza kuwa uamuzi uliotolewa na Jaji
Twaib aliamuru utekelezaji wa hoja za upande wa utetezi katika kesi hii
ya ugaidi zisikilizwe na kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Kisutu.
“Tukiendekeza hii tabia tutamaliza mahakimu wote
wa mahakama hii tunasisitiza upande wa utetezi utoe sababu za msingi za
wewe kujitoa.”Alisema Kongola.
Akijibu hoja hizo, Wakili Salim alieleza kuwa ili
haki ionekane inatendeka wewe Hakimu Liwa ujitoe ili hakimu mwingine
atoe maamuzi wa hoja zetu.
Hakimu Liwa alisema ni kweli nilikwisha toa uamuzi
wangu juu ya maombi ya washtakiwa lakini Mahakama Kuu imeona kivingine
kuwa sijatumia mamlaka yangu vizuri nakubaliana na uamuzi huo.
Lakini uamuzi huo wa Jaji Twaib haukufafanua nini
kifanyike, umetuacha hoi, ila alitoa angalizo kuwa ushahidi wa kesi
hauwezi kutoka hewani na kwamba maelezo yaliyomo katika hati ya mashtaka
ya kesi hiyo yapo sahihi.
“Kitu ambacho hata mimi nilikuwa nakishangaa ni
hii hati ya mashtaka kuletwa Tanzania Bara badala ya Visiwani, lakini
nilipoisoma sheria ya ugaidi nikabaini mtu anaweza kushtakiwa mahali
popote.” Alisema Hakimu Liwa.
إرسال تعليق