Pluijm: Yanga itakuwa balaa!


hans
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans Der Van Pluijm amesema ameingia na mfumo wa mpya wa kucheza soka ya kuvutia na kushambulia ili kuiwezesha timu hiyo kushinda mabao mengi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pluijm amechukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo ambaye mkataba wake ulisitishwa wiki, iliyopita baada ya Yanga kufungwa na Simba mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa Nani Mtani Jembe uliochezwa Desemba 13 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Pluijm alisema jambo la kwanza atakalolitia mkazo ni kuwawezesha wachezaji kucheza kitimu zaidi ili kujihakikishia ushindi katika kila mechi ya ligi hiyo.
Pluijm alisema anatarajia kufanya mabadiliko kwa muda mfupi na hilo atafanikiwa iwapo atapata ushirikiano kutoka kwa wachezaji na uongozi wa klabu hiyo.
Alisema katika mikakati yake ya ushindi atatumia mashambulizi kuanzia mabeki wa pembeni ambao watakipanda kushuka haraka ili kuweka ulinzi.
Pluijm alisema pamoja na soka lina matokeo matatu kushinda, kutoka sare na kufungwa, lakini malengo yake ni kutaka Yanga kucheza soka ya kuvutia wakipanga mashambulizi zaidi kuliko kulinda mabao.
“Nimefurahi sana kurejea Yanga najisikia kama nipo nyumbani na tayari nimeanza kazi na malengo yangu ni kutaka timu kushinda mabao mengi,” alisema Pluijm.
Alisema suala la nidhamu kwa wachezaji ni kitu muhimu katika kuijenga timu na kufanya vizuri katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.
Katika kuhakikisha malengo yake yanatimilika, Pluijm ameomba kupewa mikanda minne ya mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu mechi za ya Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar
Pluijm aliomba kupewa mkanda wa video wa mechi mbili za kirafiki za Nani Mtani Jembe za Simba na timu yake ili waweze kuangalia kabla ya timu hiyo kucheza dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga inatarajiwa kuingia kambini leo katika Hoteli ya Kiromo iliyoko Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.

Wachezaji wa timu hiyo wanatarajia kufanya mazoezi asubuhi na jioni ni kuwajenga ufiti ili waweze kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
Pluijm Machi mwaka huu, aliongoza timu hiyo vizuri katika harakati ya kuwania ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilitolewa kwa tabu na Al Ahly ya Misri.
Yanga ilitolewa kwa mikwaju ya penalti nchini Misri baada ya timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 huku Yanga ikipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani, lakini Al Ahly ilisawazisha waliporudia kwao.

Post a Comment

أحدث أقدم