
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania
watanufaika na kipato na maarifa ya teknolojia ya kisasa kutokana na ajira
ambazo watapata katika nchi ya Qatar baada ya mkataba kusainiwa hivi karibuni.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Desemba
20, 2014) jijini Doha, Qatar wakati akizumgumza na waandishi wa habari ili
kuwapa taarifa fupi juu ya mambo yaliyojiri kwenye mazungumzo yake na Waziri
Mkuu wa Qatar, Sheikh Abdulla Nasser Al Thani.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika ofisini
kwa Sheikh Abdulla, Waziri Mkuu Pinda amesema wamekubaliana kutoa ajira kwa
Watanzania kwa sababu nchi hii inahitaji wafanyakazi wengi kwenye sekta
mbalimbali na raia wake ni wachache.
“Hivi sasa wapo Watanzania wanaofanya kazi
hapa lakini ni wachache mno. Mazungumzo yalishaanza siku za nyuma. Tukisaini
mkataba katika muda mfupi ujao, tutajua ni idadi gani wanahitajika na wanaweza
kuja kila baada ya muda gani,” alifafanua Waziri Mkuu.
“Hapa Qatar kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, kwa
hiyo wanahitaji watu wa kufanya kazi... kwenye mahoteli, viwandani, na kikubwa
hapa ninachokiona watu wetu watapata kipato lakini pia watapata ujuzi kwa maana
ya maarifa yanayoendana teknolojia ya kisasa,” aliongeza.
Akeleza mambo mengine ambayo wamekubalina
kushirkiana kama nchi rafiki, Waziri Mkuu alisema kuna mambo makuu manne
likiwemo hilo la ajira. “La kwanza ni Kilimo. Hapa Qatar ni jangwa kila
mahali. Wamekubali kuja kuwekeza kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi kwa sababu
sisi tuko karibu nao zaidi kuliko Marekani au Brazil.”
“Wanaweza kupata mchele, matunda, nyama kwa maana
ya machinjio na viwanda vya kusindika nyama lakini pia katika uvuvi wa samaki.
Tunayo bahari ila mitaji yetu ni midogo. Kwa hiyo wamekubali kuangalia eneo
hilo pia,” alisema.
Alisema eneo la pili ni la gesi na mafuta.
“Wamekubali kutusaidia utaalmu ili tushirikiane nao katika namna kutumia gesi
kwenye ngazi ya chini hasa viwanda kwa sababu wenzetu wana uzoefu wa muda
mrefu. Hata kwenye mafuta wameonyesha kuwa wako tayari,” alisema.
Eneoa la tatu alilitaja kuwa ni kutoa fursa ya
ajira kwa Watanzania na la nne ni TEHAMA. “Hawa wenzetu wamechanganya TEHAMA na
sayansi na sasa wana Jiji la Sayansi na Teknolojia. Chini ya makubaliano
tutakayofikia, watu wetu watakuja kujifunza masuala ya gesi na mafuta.”
Alisema wamekubaliana na Sheikh Abdulla al Thani
kuunda timu ya pamoja baina ya nchi zao ili ifanye kazi ya kuainisha ni maeneo
gani wanataka waanze nayo kwanza kulingana na mahitaji. “Nimemuahidi nikifika
nyumbani nitaandika barua ili mchakato wa kuunda timu uanze rasmi,” alisema.
Mchana huu, Waziri Mkuu Pinda atakuwa na
mazungumzo ya Kiserikali na Mawaziri wa Kazi na Ustawi wa Jamii; Uchukuzi;
Miundombinu na Uwekezaji wa Qatar. Naibu Mawaziri atakaokutana nao ni wa Uchumi
na wa Nishati.
Jioni Waziri Mkuu amepangiwa
kukutana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar (Qatar Business
Community), wajumbe wa Chama cha Wafanyabiashara cha Qatar (Chamber of Commerce
of the State of Qatar) na pia atakutana na Watanzania waishio Qatar. Kesho
(jumatatu, Desemba 22, 2014) atatembelea Mamlaka ya Bandari ya Qatar na makao
makuu ya kampuni ya uchimbaji gesi ya Qatar.
Waziri Mkuu amefuatana na
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kimani; Waziri wa Kilimo na
Maliasili wa Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati, Bw.
Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Godfrey
Zambi.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Bw. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego, wabunge
wawili Bi. Amina Makilagi na Bw. Aeshy Hilali, Dk. Gideon Kaunda wa TPSF na Bw.
Shigela Malocha kutoka TPDC.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
S. L. P.
3021,
DAR ES
SALAAM.
JUMAPILI,
DESEMBA 21, 2014
إرسال تعليق