Dar es Salaam. Pamoja na maelezo ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa
juzi juu ya ugonjwa wa saratani ya tezi dume mara baada ya kurejea
nchini kutoka Marekani alikotibiwa, maswali kuhusu ugonjwa huo bado ni
mengi na hivyo kuhitaji ufafanuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini,
Rais Kikwete alielezea hali yake, jinsi alivyogundulika kuwa na saratani
ya tezi dume na matibabu aliyoyapata.
Rais Kikwete anastahili pongezi kwa namna
alivyovunja ukimya na amesaidia kujua umuhimu wa kujali afya zetu na
kuweka wazi hali zetu za kiafya, si kwa tezi dume pekee, bali pia
maradhi mengine.
Maana ya saratani
Saratani maana yake ni ukuaji holela bila
mpangilio wa seli baada ya kuparanganyika kwa mfumo wa seli unaodhibiti
ukuaji na uhai wake. Na uvimbe wa kawaida wa tezi maana yake ni kuwa
seli zimetutumka tu lakini hakuna mparanganyiko wa seli wala kukua kwa
kusambaa kiholela kama ilivyo kwa saratani.
Hivyo, ndio maana kuna tatizo la kuvimba tezi dume na wengine kupata saratani ya tezi dume kwa wanaume wenye umri mkubwa.
Tezi dume ni sehemu mojawapo ya mfumo wa uzazi wa
kiume. Inaundwa na sehemu mbili ambazo zimeunganishwa na kufunikwa kwa
nje kwa utando wa tishu.
Tezi hii ipo mbele kidogo ya puru (rectum) na
chini kidogo ya kibofu cha mkojo. Tezi dume inauzunguka mrija
unaounganisha kibofu cha mkojo na uume (urethra).
Kazi ya tezi dume
Mojawapo ya kazi za tezi dume ni kutoa majimaji
yanayochanganyika na mbegu za kiume (sperms) wakati wa kilele cha tendo
la kujamiana. Mchanganyiko huu wa mbegu pamoja na majimaji hayo
hutengeneza shahawa (semen).
Majimaji hayo husaidia kuzipa mbegu za kiume nguvu
ya kusafiri kwenye uke mpaka kufikia kwenye mirija ya uzazi, tayari kwa
utungisho na yai la kike. Vilevile husaidia kupunguza hali ya
kitindikali iliyopo katika uke, ambayo isiporekebishwa, huua mbegu
nyingi za kiume na kufanya utungisho kuwa wa tabu.
Saratani ya tezi dume inashika nafasi ya tatu kwa
kusababisha vifo vinavyotokana na saratani kwa wanaume wa umri
mbalimbali duniani.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق