Dar es Salaam. Viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC),
Zitto Kabwe na Deo Filikunjombe wamemtuhumu Waziri William Lukuvi kuwa
alitaka kuiba ripoti ya kamati yao kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni
kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hilo lilihitimishwa Jumamosi wakati Bunge
lilipoazimia kuwajibishwa kwa watu wote waliohusika kwenye uchotwaji wa
fedha hizo, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa taasisi
za fedha zilizoruhusu kufanyika kwa miamala mikubwa kinyume na taratibu
za kibenki. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao wawili
kutoka Chadema na CCM walilieleza gazeti hili kuwa jaribio hilo
lilishindikana baada ya wao na mjumbe mwalikwa, Luhanga Mpina (CCM)
kuamua kukesha wakiilinda ripoti hiyo tangu ilipokuwa ikichapwa hadi
ilipowasilishwa bungeni.
Hata hivyo, Lukuvi alikanusha vikali tuhuma hizo
akisema kuwa aliipata ripoti hiyo siku iliposomwa na kwamba kama
angehusika, asingekubaliwa kuwa mjumbe wa kamati ya maridhiano
iliyoundwa mwishoni mwa kikao kupendekeza maazimio ya Bunge.
“Si kweli,” alisema waziri huyo wa nchi anayehusika na sera, utaratibu na Bunge.
“Unajua PAC walikuwa wanafanya kazi chini ya
hazina. Hata Spika wa Bunge hakuiona hiyo ripoti, aliisikia tu ikisomwa
bungeni. Kwanza kamati ilikuwa ikidurufu hiyo taarifa yake eneo la mbali
na ili uipate ilikuwa ni lazima umrubuni Zitto.”
Aliongeza kusema: “Kama kweli nilikuwa nataka
kuiba taarifa yao nisingekubali kuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ya
maridhiano, iliyokutana kupitia upya mapendekezo ya PAC baada ya yale ya
awali kuzua mvutano bungeni.”
Hata hivyo, Filikunjombe, ambaye alikuwa makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo, alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa
walilazimika kumwondoa eneo la kuchapishia ripoti hiyo. “Waziri Lukuvi
alitumwa saa 9:00 usiku kuiba taarifa yetu wakati tunaichapa. Taarifa
ilikuwa katika ‘flash’ na tulipogundua hilo tulimfukuza. Sisi tuliamua
kuilinda ripoti ili isiibwe,” alisema Filikunjombe ambaye ni mbunge wa
Ludewa kwa tiketi ya CCM.
“Ile taarifa tuliichapa usiku wa kuamkia Jumatano
ambayo ilikuwa siku ya kuiwasilisha bungeni. Na hiyo ndiyo ilikuwa
sababu ya kikao cha Bunge kuahirishwa mara tu baada ya PAC kuwasilisha
taarifa yake, ili Serikali ikajipange,” aliongeza.
Mbali na kauli yake ya jana, Filikunjombe aligusia
suala hilo la ulinzi wakati akishukuru wabunge kwa kushikamana katika
kufikia maazimio manane ya kuwawajibisha wote waliohusika.
Katika shukrani hizo, Filikunjombe alisema
walilazimika kukesha usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kuilinda ripoti
yao isiibiwe na hivyo kuwashukuru watendaji wa Bunge kwa kazi nzuri.
Hata hivyo, kabla ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo
kulienea taarifa kuna watu waliiiba na kunyofoa kurasa zilizokuwa na
nyaraka za vielelezo na baadaye kuanza kuzisambaza. Polisi ilidai
baadaye kuwa ilimkamata mtu aliyekuwa akisambaza vitabu hivyo vya
ripoti, lakini hadi leo hajafikishwa mahakamani wala hakuna taarifa
yoyote iliyotolewa na polisi kuhusu maendeleo ya mtuhumiwa huyo.
Katika sakata hilo kubwa la aina yake, Bunge
limtia hatiani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati, Eliachim Maswi na wakurugenzi wa Shirika la Umeme kwa kuhusika
kwa makusudi au kwa uzembe katika kufanikisha miamala haramu kutoka
kwenye akaunti hiyo.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق