Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amelalamikia uamuzi wa Bunge unaopendekeza yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua, akidai kuwa haukuwa wa haki kwa wote waliotuhumiwa na ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.
Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa
mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306
bilioni kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe
kwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya
kukata kodi.
Jaji huyo hakusalimu amri wakati Bunge likijadili
tuhuma dhidi yake, akisema anaamini alichofanya na kutaka abebeshwe
msalaba na wakati fulani alishiriki kupendekeza jinsi ya kufikia
maazimio ya Bunge dhidi ya watuhumiwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu maazimio ya Bunge katika sakata la uchotaji wa fedha hizo, jaji Werema alisema:
“Kilichofanywa na Bunge ni mob justice (uamuzi wa
kufuata mkumbo) kwa sababu hata waliowatuhumu, hawakupewa nafasi ya
kujieleza. (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna)
Tibaijuka na (mmiliki wa hisa za IPTL, James) Rugemalira hawakusikilizwa
lakini wamehukumiwa… ilionekana dhahiri jinsi Bunge linavyoingilia
uhuru wa Mahakama kwa kutoizingatia hukumu ya Jaji (John) Utamwa,”
alisema Jaji Werema.
“There was no justice at all (hakukuwa na haki
kabisa). Bado haijathibitika ukweli kuhusu fedha zile kama ni za umma au
la. Ninyi waandishi bado mna nafasi ya kufanya uchunguzi ili muwaeleze
wananchi ukweli kuhusu wasichokijua,” alisema Werema ambaye mara nyingi
hukataa kuzungumza na waandishi wa habari siku za Jumapili kwa madai ya
kupumzika.
Werema alitaka pia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iueleze umma ili kuondoa sintofahamu
iliyopo juu ya mmiliki halali wa fedha zilizokuwamo katika akaunti hiyo.
Kauli ya Jaji Werema inafanana na iliyotolewa na
Waziri Tibaijuka kupitia gazeti hili jana akisema anasikitika kwa kuwa
hakupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma za kunufaika na fedha hizo.
Tibaijuka pia alisema anashangaa jinsi gani jina
lake liliingizwa kwenye ripoti ya Kamati ya PAC, wakati halikuwapo
katika ripoti ya CAG.
Juzi Bunge lilihitimisha mjadala wa kashfa ya
akaunti ya Tegeta Escrow, kwa kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja
na kuwawajibisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Bunge hilo pia liliwawajibisha wajumbe wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Shirika la Umeme (Tanesco) na liliwavua nyadhifa zao
wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni mwenyekiti wa
Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge.
Akisoma maazimio hayo juzi, Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema kuwa
baadhi ya watu waliochukua fedha hizo ni viongozi wa umma na maofisa wa
Serikali kama mawaziri, majaji, wabunge, wenyeviti wa kamati za Bunge,
wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na
watu binafsi.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق