Sheria kubana utitiri kampuni za ulinzi yaja

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema sheria mpya ya kusimamia kampuni binafsi za ulinzi itatungwa na Bunge mwakani. Sheria hiyo ikipitishwa imeelezewa kuwa itasaidia kupunguza utitiri wa kampuni hizo zinazofikia 750 hivi sasa.
Akizungumza jana, Dar es Salaam, Mratibu wa Sekta Binafsi yaUlinzi wa Jeshi la Polisi, Adam Maro alisema maandalizi ya sheria hiyo yameshakamilika na kinachosubiriwa ni kupelekwa bungeni.
Alisema licha ya kuwapo kwa idadi kubwa ya kampuni za ulinzi, nyingi zinafanya kazi bila kufuata utaratibu ikiwamo wa kuajiri wafanyakazi wazee na kuwalipa wafanykazi wao mishahara isiyostahili.
Akimwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu katika sherehe za Kampuni ya Ulinzi ya Security Group Afrika (SGA) iliyotimiza miaka 30, Maro alisema sheria hiyo itakuwa silaha ya kudhibiti kampuni zisizofuata sheria, kanuni na utaratibu.
“Kampuni nyingi hazina vifaa vya kutosha, matokeo yake zinashindwa kupambana na wahalifu na kusababisha hasara kwa wateja,” alisema Maro.
Alisema kutungwa kwa sheria hiyo kutazifanya kampuni nyingi ziungane ili ziwe na mitaji mikubwa itakayowawezesha kuwa na vifaa vya kisasa.
“Utashangaa mtu ana mtaji Sh3 milioni anataka kusajili kampuni ya , matokeo yake unakuta wanalinda kwa kutumia svirungu,” alisema Maro.
Alisema Tanzania inazihitaji kampuni binafsi za ulinzi kwa kuwa kuna upungufu wa askari polisi ambao kwa sasa kila askari mmoja analinda watu 1,100 badala ya 450, lakini nyingi hazina msaada hivyo kuongeza mzigo kwa Jeshi la Polisi badala ya kusaidia.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa SGA, Eric Sambu alisema changamoto zinazoikabili kampuni hiyo ni msongamano wa magari ambao husababisha kuchelewa kufika katika matukio.
“Barabara bado zinajengwa, nyingine zimefungwa ili kupisha ujenzi, hiyo ni changamoto kubwa inayosababisha tushindwe kufika kwenye matukio kwa wakati,” alisema.

Post a Comment

أحدث أقدم