Na Shukri Mohamed, Mogadishu
Utawala wa mpya wa Muda wa Kusini Magharibi mwa Somalia (ISWA) unatafuta
suluhisho la haraka la hali iliyopo ya kukosekana kwa usalama na
unafanya kazi katika kuileta jamii pamoja ambayo awali ilipinga uundwaji
wake.
Rais wa Utawala wa Muda wa Kusini
Magharibi Sharif Hassan Sheikh Adan akihutubia umati wa watu wakati wa
mkutano uliofanyika tarehe 20 Disemba pamoja na viongozi na wazee wa
ndani huko Barawe. [UN Photo/ Ilyas Ahmed]
Tarehe 17 Novemba, wajumbe kutoka mikoa ya Bay, Bakol na Shabelle ya
Chini walimchagua aliyekuwa spika wa bunge la serikali ya mpito ya
shirikisho Sharif Hassan Sheikh Adan kuwa rais wa dola mpya ya
shirikisho kwa kipindi cha miaka minne.
Lakini kabla ya kuchaguliwa kwa Adan, jambo ambalo lilipokelewa vizuri
na serikali ya shirikisho ya Somalia na wadau wa kimataifa, kulikuwa na
malalamiko Baidoa, kupinga nafasi ya utawala mpya.
Wasiwasi ulikuwa unahusiana na madai ya kambi mbili za upinzani ambazo
kila moja ilihamasisha uundwaji wa dola ya mikoa sita na dola ya mikoa
mitatu, ambapo kila moja ilitaka kuwa na rais wake.
Baada ya mazungumzo kadhaa yaliyosimamiwa na serikali ya shirikisho,
kambi ya mikoa sita, inayoongozwa na Madobe Nunow Mohamed, ilikubali
kuridhia dola ya mikoa mitatu na kuingia katikamakubaliano ya
kushirikiana madaraka.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, viongozi kutoka katika utawala wa mikoa
sita, ambao pia unajumuisha Gedo, Jubba ya Chini na Jubba ya Kati,
watahudumu nafasi ya makamu wa rais na spika wa bunge katika ISWA.
Mikoa ya Gedo, Jubba ya Chini na Jubba ya Kati tayari zilishaunda
Utawala wa Muda wa Jubba, ambao una matatizo madogo yake yenyewe
ulioundwa chini ya mfumo wa serikali ya shirikisho.
Wanazuoni na wazee kutoka kambi inayounga mkono utawala wa mikoa sita
wanahitaji kutulizwa kisiasa, alisema Ibrahim Muse Herow, mkuu wa Chama
cha Wanazuoni wa Bay na Bakol, kikundi cha wataalamu kutoka nyanja
mbalimbaliu ambao wanafanya kazi kwenye masuala yanayohusiana na
maridhiano na utawala.
"Uanzishaji wa utawala huo ulipingwa ," Herow aliiambia Sabahi. "Baadhi
waliunga mkono mikoa sita na baadhi walitaka mikoa mitatu, na mpaka sasa
hakukuwa na suluhisho kamili. Hata hivyo, inaonekana kama kwamba kambi
ya Sharif Hassan imeenea na inapokea msaada wa serikali na wa jumuiya ya
kimataifa."
Utawala mpya unaweza kufanikiwa kama utachukua hatua sahihi, alisema.
"Sharif Hassan inabidi ateue baraza la mawaziri ambalo lina uwiano na
kuridhisha koo zote kwa kuwa kwa sasa Somalia inashirikiana madaraka kwa
kuzingatia koo," Herow alisema.
"Mikoa hii pia inapata ukame unaojirudia na njaa ambayo inasababisha
vifo vya mamia ya watu kila mwaka. Utawala mpya inabidi uje na mpango wa
kuwaokoa watu wanaokufa," alisema.
ISWA kwa sasa inakamilisha muundo wake wa utawala, kuteua mawaziri wake
na wakurugenzi wa ofisi za umma, na baadaye itaendelea katika kuunda
utawala wa wilaya, alisema msemaji wa ISWA Siad Sheikh Dahir.
"Wakati uteuzi wa mawaziri na watawala wa wilaya utakapokamilika,
inabidi tukabiliane na kazi muhimu sana, ambayo ni kuboresha maisha ya
watu na utafutaji riziki wa msingi," aliiambia Sabahi.
Utawala utafanya kazi ya kurudisha miundombinu ya umma iliyoharibika
wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, kama vile shule, barabara na
hospitali, alisema. Pia unapanga kurudisha usalama na kukomboa miji
ambayo bado iko chini ya udhibiti wa al-Shabaab.
Mkaazi wa Baidoa Abukar Sidow, mwenye miaka 34, alisema alifurahi
aliposikia kwamba pande mbili zinazopingana zimefikia makubaliano na
sasa zinalenga kujenga upya mikoa mitatu.
"Baidoa ilikuwa katika hatari ya kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa
wenyewe, na kulikuwa na kutoelewana kwa kiasi kikubwa katika utawala,"
aliiambia Sabahi. "Lakini sasa hali inaonekana kutulia, na watu wote
wameelekeza macho yao kwenye utawala mpya na matumaini makubwa ya
kubadili mazingira ya kisiasa na hali ya maisha katika mikoa hiyo."
Sidow aliiomba serikali ya shirikisho kuongeza mara mbili msaada wake
kwa ajili ya taifa jipya ili mfumo wa shirikisho uweze kufaulu na
Somalia iweze kufanya uchaguzi mwaka 2016.
Chanzo: sabahionline.com
إرسال تعليق