84 kizimbani vurugu Udom, Serikali yajisafisha

Dodoma. Wanafunzi 84 wa programu maalum ya stashahada ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dodoma(udom) waliofanya mgomo na kuandamana kushinikiza kulipwa madai yao, juzi wamepandishwa kizimbani kwa kosa la kukusanyika bila kibali maalum.
Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana walifanya mgomo huo juzi na kuandamana  kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha madai yao.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma Kabate Richard, mwendesha mashitaka Lopa, aliiambia mahakama kuwa  wanafunzi hao walitenda kosa hilo juzi majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri.
Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi manne ya kesi namba 5, 6,7 na 8 ya mwaka 2015 ambapo wanakabiliwa na kosa hilo.
Hakimu huyo baada ya kesi hiyo kusomwa aliwapa dhamana ambapo wanafunzi hao walijidhamini wenyewe kwa shilingi elfu ishirini, ishirini kauli ya maneno.
Wanafunzi hao wapo nje kwa dhamana ambapo kesi zao zimepangwa kusikiliza  tarehe 16-19 februari mwaka huu.
Kufuatia uvumi ulioenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii na katika mji wa Dodoma na viunga vyake kuwa kuna wanafunzi waliofariki dunia kufuatia maandamano yaliyofanyika juzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassor Mzee amesema kuwa taarifa hizo si za kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mjini hapa, Dk Mzee amesema kuwa hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma iliyopokelewa katika hospitali hiyo na kusisitiza kuwa taarifa hizo siyo za kweli.
“Hapa hospitalini hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa Udom na hata baada ya kupata taarifa hizo nilikwenda mapokezi kwa ajili ya kupata taarifa na kwenye wodi zote hapa hospitalini lakini hakuna mwanafunzi hata mmoja wa kutoka Udom aliyefika hapa kutibiwa,” amesema Dk Mzee.
Aliongeza kuwa, “Hata kwenye chumba cha kuhifadhia maiti hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa udom… labda kama waliamua kwenda kuzihifadhi maiti hizo kwenye hospitali nyingine nje ya hapa lakini hapa hakuna maiti yoyote kutoka Udom.”
Awali baadhi ya wanafunzi waliokuwa kwenye maandamano ya kudai fedha zao za kujikimu walidai kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wenzao waligongwa na gari ya polisi iliyokuwa ikitawanya maandamano hayo ambayo polisi waliyaita ni haramu na kufariki dunia.
Pia katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa juzi na jeshi la polisi haikutaja vifo wala majeruhi zaidi ya kutaja idadi ya wanafunzi waliotiwa mbaroni kufuatia maandamano hayo kuwa ni 84.

Post a Comment

Previous Post Next Post