Dar es Salaam. Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Eusebius Nzigilwa amevunja ukimya akisema ni kweli alipokea Sh40.4
milioni kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalira zikiwa
matoleo ya kusaidia uendeshaji wa kanisa.
Askofu Nzigilwa ni mmoja wa watu waliopata fedha
kutoka kwa Rugemalira anayehusishwa kugawa kwa watu mbalimbali mabilioni
ya shilingi yanayohusishwa na fedha zilizochotwa katika Akaunti ya
Tegeta Escrow wakiwamo wabunge, mawaziri na viongozi wa dini.
Tayari baadhi ya viongozi wa Serikali wamewajibika
kwa ama kutumia vibaya madaraka yao au kupokea fedha hizo kinyume cha
sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Kupitia taarifa yake ya kurasa tatu kwa vyombo vya
habari, Askofu Nzigilwa alielezea uhusiano wake na familia ya
Rugemalira ulivyoanza na jinsi ambavyo amekuwa akitoa sadaka na michango
mbalimbali ya hali na mali.
“Kanisa linategemezwa na nguvu ya Roho Mtakatifu
anayeliongoza kupitia michango ya watu. Hivyo, kwa waumini kutoa
michango na matoleo kwa kanisa na watumishi wake ni jambo la kawaida
katika desturi za imani yetu tangu nyakati za mitume,” alisema askofu
huyo.
Alisema uhusiano wake na familia ya Rugemalira
ulianza mwaka 2008 alipopangiwa katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa
Rozari Takatifu, Makongo Juu akiwa Paroko Msaidizi, Rugemalira akiwa
muumini katika parokia hiyo.
Alisema akiwa katika parokia hiyo, walikuwa na
ujenzi wa nyumba ya mapadri na mikakati ya ujenzi wa kanisa jipya la
parokia hiyo na katika shughuli zote hizo, Rugemalira na waumini wengine
walikuwa ni wachangiaji wazuri.
“Hata baada ya kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi
tumekuwa tunashirikiana na kuwasiliana na familia ya Rugemalira katika
masuala mbalimbali ya kikanisa na kijamii,” alisema.
Mamilioni yaingia
Kuhusu fedha hizo, Askofu Nzigilwa alisema katika
moja ya mawasiliano yao Februari mwaka jana, Rugemalira alimuomba namba
ya akaunti yake ya Benki ya Mkombozi ili aweke matoleo yake... “Kwa
kuniomba akaunti hiyo nilijua anataka kuweka matoleo ya fedha; lakini
kiasi alichokuwa amenuia kukiweka sikukijua mpaka nilipoangalia Bank
Statement na kuona kampuni ya VIP Engineering imeingiza Sh40.4 milioni
katika akaunti hiyo Februari 27, 2014.
“Niliwasiliana na Ndugu Rugemalira na kumwambia
nimeona kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yangu; naye akaniambia
hayo ni matoleo ambayo anaamini yatasaidia katika shughuli zetu za
kitume na kichungaji. Nikamshukuru kwa ukarimu huo mkubwa,” alisema.
Alisema matoleo hayo yalipokewa kwa moyo mnyofu
kutoka kwa mtu anayefahamika kwa ukarimu wake katika kusaidia Kanisa na
watumishi wake.
Post a Comment