Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imebainisha kuwa hadi kufikia
Machi mwaka huu, bei ya mafuta nchini itaendelea kushuka kulingana na
kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Hata
hivyo, mamlaka hiyo imeonya kuwa bei hiyo ya mafuta nchini haitaweza
kupungua kwa kiasi kikubwa, kutokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi
dhidi ya dola ya Marekani pamoja na kutokubadilika kwa ushuru mbalimbali
wa ndani wa mafuta.
Pamoja
na hayo, Kampuni ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PICL) imeiomba
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini kuingilia kati na
kuihamasisha Serikali iongeze ulinzi katika mabomba na matangi ya mafuta
Kurasini, ambayo kwa sasa hayako salama na ni hatari kwa wakazi wa jiji
la Dar es Salaam.
Akiwasilisha
taarifa ya ukokotoaji wa mafuta kwa kamati hiyo Dar es Salaam jana,
Mtaalamu kutoka EWURA, Lorivii Long’idu, alikiri kuwa ni kweli kwa sasa
bei ya mafuta katika soko la dunia imekuwa ikishuka kwa kasi
ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
“Bei
hizi zimeshuka kutoka dola 100 hadi kufikia dola 60 kwa pipa ambayo ni
sawa na asilimia 40 kutokana na kudorora kwa uchumi wa bara la Ulaya
katika kipindi hiki na kuwepo kwa tofauti za mitazamo ya kisiasa hasa
katika nchi za Marekani na Urusi,” alisema Long’idu.
Hata
hivyo, alisema pamoja na bei hizo kushuka tangu Julai hadi Desemba
mwaka jana, kwa kawaida kwa Tanzania huchukua takribani miezi miwili bei
hiyo kuweza kufikia soko la ndani.
Alisema
bei zote za mafuta katika soko la ndani, zimekuwa zikishuka kuanzia
robo ya mwisho wa mwaka jana sambamba na kushuka katika soko la dunia na
kwamba bei hizo hukokotolewa na Ewura kwa kutumia kanuni maalum,
inayotumia gharama halisi za uagizaji mafuta nchini, zinazotokana na
meli za mafuta yaliyopokelewa mwezi husika yaliyonunuliwa mwezi wa nyuma
yake.
Alisema
uhusiano wa bei za soko la dunia na soko la ndani, unapishana kwa miezi
miwili na kwamba mafuta yanayotumika mwezi huu, Ewura ilikokotoa bei
zake tangu Novemba kulingana na bei ya mafuta yaliyonunuliwa katika soko
la dunia mwezi huo.
Long’idu
alisema kwa hali ilivyo sasa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia,
zitaendelea kushuka kama hakutakuwa na tukio lisilo la kawaida duniani,
hali itakayochangia kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la ndani
japo si kwa kiwango sawia.
Alisema
pamoja na bei kushuka katika soko la dunia kwa kiwango chochote kile,
bei ya ndani itashuka kulingana na thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya
Marekani lakini pia ushuru uliopo ambao katika petroli unatozwa Sh 878,
dizeli Sh 754 na mafuta ya taa Sh 701 kwa lita ambao wenyewe
haubadiliki.
Kwa
upande wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Nishati na Madini, Jerome
Bwanausi, aliagiza Ewura na PICL wanapokokotoa bei za mafuta
kuhakikisha wanatoa ufafanuzi wa hali halisi ya bei za soko la dunia na
utaratibu mzima wa uingizaji wa mafuta nchini ili kuondoa habari potofu
zinazosambazwa juu ya bei hizo za mafuta.
Aidha,
aliagiza Wizara ya Nishati na Madini kuchukua hatua za haraka na
kushughulikia suala la ulinzi katika mabomba na matangi ya mafuta ili
kudhibiti hali ya hatari ya kulipuliwa kwa matangi hayo na kuhatarisha
usalama wa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
“Hii
ni hatari sana kwa namna yale mabomba yalivyo hayana ulinzi, watu
wanatoboa mabomba na kuiba mafuta na kuweka maboya, endapo mtu yeyote
akitupa moto pale Dar es Salaam nzima itakuwa haipo, hatua za haraka
zichukuliwe, na kamati ipatiwe taarifa za ulinzi wa sasa katika eneo
hilo,” alisisitiza.
Aidha,
alisema kutokana na hali ya hatari ya usafirishaji wa mafuta iliyopo
sasa kupitia malori hasa katika vijiji malori hayo yanakopita na kulala,
ni vyema Serikali ikaanza mchakato wa kuchimba mabomba ya kusafirishia
mafuta na kufufua reli ili kudhibiti usalama wa wananchi
إرسال تعليق