Watu
wasiojulikana wamelichoma moto na kuliteketeza Kanisa la Evangelical
Assemblies of God wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma na kuteketekeza kila
kitu kilichokuwemo ndani ya kanisa hilo.
Mkuu
wa Wilaya ya Kibondo, Venance Mwamoto amesema kuwa tukio hilo la
mwanzoni mwa wiki hii, limeacha athari kubwa za mali na kwamba hakuna
mtu yeyote ambaye amepata madhara kuhusiana na uharibifu.
Mwamoto ambaye ni Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kakonko, alisema kuwa bado haijajulikana hasa sababu ya kuchomwa kwa kanisa hilo.
Lakini,
alibainisha kuwa sababu mbili kubwa, ikiwemo ya mgawanyiko wa viongozi
na masuala ya kisiasa yanaweza kuwa chanzo cha tatizo hilo.
Alisema
zipo taarifa za masuala ya kisiasa kufanywa na baadhi ya viongozi wa
kanisa hilo, ikiwemo vyombo vilivyokuwa vinatumika kwenye kampeni kwa
mgombea wa uenyekiti wa kijiji hicho kupitia chama cha NCCR – Mageuzi,
ambaye ni kiongozi wa kanisa na ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
kijiji.
Alisema kuwa masuala hayo ya siasa na mgogoro wa viongozi wa kanisa, yanafanyiwa kazi kwa kina ili kubaini ukweli.
Alisema
kwamba kiongozi mmoja wa kanisa hilo, anashikiliwa na vyombo vya ulinzi
na usalama akituhumiwa kuhusiana na uchomaji huo .
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Kigoma, Jafari Mohammed alithibitisha tukio hilo na
kwamba uchunguzi kujua sababu hasa za kuchomwa kwa kanisa hilo,
unaendelea.
إرسال تعليق