CUF: CCM wamemdanganya Kinana

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana
Chama Cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Tanga, kimesema kuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, wamemdanganya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana, kuwa wanachama 216 wa CUF wamehamia CCM.
Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Mwenezi na Itikadi  wa CCM Mkoa wa Tanga, Mathew Mganga, kumwambia Kinana katika mkutano wa hadhara uwanja wa Tangamano  kwamba kuna wanachama 216 wa CUF wamehamia CCM ambao wote wanaishi mji wa Pongwe.

Mbaraka Sadi, alijitokeza na kuidai kwamba ametoka CUF na sasa anajiunga na CCM na alikuwa anawawakilisha wanachama wenzake 216 ambao
wametoka CUF na kuhamia CCM wote wakazi mji wa Pongwe wilayani Tanga.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tanga, Rashidi Jumbe, alisema kuwa amepuuza uongo huo na kwamba viongozi wa CCM Mkoa wa
Tanga wamemdanganya Kinana.

Alisema kuwa hakuna hata mwanachama mmoja wa CUF aliyehamia CCM bali huo ni upuuzi na uongo.

Alisema katika mkutano huo hakukuwa hata na wanachama 10 waliojitokeza wakidai wanarejesha kadi za CUF na kujiunga na CCM.

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu Uongozi CUF Taifa, Nuru Awadh, alisema kuwa mwanachama wa CUF aliyehamia CCM ni mmoja tu aliyemtaja kuwa ni Mbaraka Sadi na mwingine kutoka Chadema, Kassim Makubeli.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم