Mauaji haya ya vikongwe yadhibitiwe

Katuni.
Kumekuwepo na matukio ya kujirudia kila mara kuhusiana na mauaji ya vikongwe na watu wengine wasio na hatia kutokana na imani potofu za kishirikina.
Matukio haya yamekuwa yakitokea maeneo mengi nchini, lakini zaidi katika mikoa ya kanda ya ziwa. Katika unyama huo, waathirika wakubwa huwa ni vikongwe. Na kwa bahati mbaya, walengwa zaidi ni vikongwe akina mama ingawa hata wanaume wazee pia huuawa kwa sababu hizi zisizokuwa na mashiko.

Kwa mfano, katika toleo letu la jana, kulikuwa na taarifa za kuwapo kwa matukio 112 ya mauaji yanayohusiana na imani za kishirikina pamoja na ugomvi wa mali za mirathi kwenye mkoa wa Simiyu pekee kati ya miezi ya Januari hadi Desemba mwaka jana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, ni kwamba licha ya kuwapo kwa idadi hiyo kubwa ya matukio ya mauaji, bado idadi hiyo ni nafuu kulinganisha na mwaka 2013 ambao ulikuwa na matukio 121.

Kamanda Mkumbo alieleza kuwa kupungua huko kulitokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na jeshi lake katika kuwakamata watuhimiwa kwa haraka pamoja na elimu ya utii wa sheria bila shuruti inayoendelea kutolewa kwa jamii. Sisi tunapongeza jitihada hizi, hasa kutokana na imani yetu kwamba jambo lolote huwa na mahala pa kuanzia na hivyo kupungua huko kwa matukio takriban tisa katika mwaka uliopita kulinganisha na mwaka 2013 ni hatua inayoonyesha mwelekeo chanya katika vita hiyo.

Hata hivyo, sisi tunadhani kuna haja ya kuangalia zaidi eneo hili. Kwamba, jitihada zaidi ziongezwe kwani hali hii ya kuendelea kuuawa kwa watu wasiokuwa na hatia haikubaliki kwa namna yoyote ile.

Tunaingiwa hofu kwamba, kama mkoa mmoja tu wa Simiyu umeendelea kuwa na matukio ya mauaji yanayozidi idadi ya mia moja kwa mwaka mmoja, ni wazi kwamba upo uwezekano wa kuwa na maafa makubwa zaidi katika mikoa mingine ya ukanda wa ziwa kama Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara na Kagera. Na idadi ya wafu watokanao na imani za kishirikina katika mikoa hiyo ikichangnywa kwa pamoja na mikoa mingine nchini, ni wazi kwamba itakuwa kubwa kiasi cha kuogofya. Hili halivumiliki hata kidogo.

Ni kwa sababu hiyo, ndipo sisi tunapoona kuna haja ya kukumbushia tena na tena juu ya umuhimu wa kuendelea kupiga vita matendo haya ya kinyama bila kuchoka. Na ikibidi,  vita hii iwe endelevu. Kila uchao iwe ikiendelezwa, tena wapambanaji wakipaza sauti zao juu zaidi na kutekeleza kivitendo kila maazimio yanayofikiwa katika kusaka ushindi dhidi ya unyama huu.

Watu wote nchini, wakiwamo wa maeneo ya Kanda ya Ziwa, wanapaswa kutambua juu ya umuhimu wa kuzingatia haki ya kuishi ambayo ni mojawapo kati ya haki kuu za msingi kwa kila mwanadamu. Ndiyo maana mara kwa mara NIPASHE tumekuwa mstari wa mbele kupiga vita vitendo hivi.

Ni muhimu ikakumbukwa vilevile kuwa mauaji kama haya yamekuwa yakisababisha huzuni kubwa kwa familia husika na pia kulitia aibu taifa katika jamii ya kimataifa. Wanaouawa ni wazee ambao huacha msiba mkubwa huku familia zao zikiteseka. Wapo watoto ambao wazazi wao wameshauawa kwa sababu hizi zisizokuwa na mashiko na hivi sasa wamebaki yatima na wanaishi maisha ya tabu na dhiki tupu.

Sisi tunadhani kwamba, wakati sasa umefika kwa serikali kukaa chini na kutafakari kwa kina jinsi ya kulikabili tatizo hilo ili kuleta amani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kama Simiyu na pia katika maeneo mengine nchini. Aidha, jamii pia inapaswa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono vita hii kwa msaslahi yao na taifa.

Msisitizo ni kwamba kila binadamu anayo haki ya kuishi na kwa msingi huo, hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kutoa uhai wa mwenzake. Na inapotokea hivyo, basi kila aliyehusika na mauaji anapaswa ashughulikiwe kikamilifu kulingana na sheria za nchi.

Tunatoa wito kwa vyombo vya usalama kujipanga zaidi ili kuhakikisha kwamba mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yanakomeshwa haraka na dunia nzima itambue kwamba Tanzania inajali na kuheshimu uhai wa kila binadamu.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم