Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM, itakuwa na vikao vizito
kuanzia Jumatatu kujadili masuala mbalimbali yanayokikabili chama hicho.
Mambo makubwa yanayotarajiwa kuchukua nafasi
katika vikao hivyo vitakavyoanza saa 72 zijazo ni kuwajadili wanachama
wake ambao baadhi ni mawaziri waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow na tathmini ya wanachama wake sita walio katika adhabu ya mwaka
mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kudaiwa kufanya kampeni za urais kabla
ya muda.
Pia kamati hiyo, inatarajia kutumia vikao hivyo
kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika na wananchi kuelekea
kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa
kuipa CCM ushindi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga hivi
karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alisema chama hicho
kitaanza rasmi vikao vyake vya ngazi ya Taifa kupitia masuala mbalimbali
yanayokihusu.
Alipoulizwa kuhusu agenda hizo katika vikao hivyo
jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu na
kusema hakuna kitu kama hicho... “Hata mkiiandika vibaya CCM, itashinda
tu,” na kisha kukata simu. Hata hivyo, habari zilizopatikana jana jioni
kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa sekretarieti ya chama hicho,
inakutana leo mjini Dodoma kuandaa ajenda za kikao hicho kitakachoanza
Jumatatu ijayo.
Mawaziri waliokumbwa na kashfa ya escrow ni Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
ni pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye nafasi
yake ya uwaziri baada ya kukiri kupewa Sh1.6 bilioni na Mkurugenzi wa
VIP Engineering, James Rugemalila.
Wengine waliotajwa kupewa mgawo na Rugemalila ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja.
Pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo yupo katika uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo.
Mbali na wahusika wa Akaunti ya Escrow, kikao
hicho cha Kamati Kuu ya CCM kitachunguza maadili ya viongozi wakiwamo
waliokumbwa na zuio la kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku
mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa.
Watakaojadiliwa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi, Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
- Mwananchi
- Mwananchi

إرسال تعليق