KAMPENI KUHUSU KATIBA MPYA ZIKIANZA, KILA LISEMWALO TULIPIME

Mchungaji Christopher Mtikila.
MWANDISHI  Eric Shigongo/UWAZI
Tangu mjadala wa mabadiliko ya Katiba ulipoanzishwa na kupitishwa bungeni, kumekuwa na matabaka mawili, moja likitaka katiba iliyoandikwa iungwe mkono na wananchi jingine likidai imechakachuliwa hivyo haifai.
Lakini Bunge Maalum la Katiba limeshapitisha katiba hiyo na kilichobaki sasa ni kampeni ambayo itahusisha pande hizo mbili.Ni jukumu la Watanzania kuamua baada ya kusikia hoja za pande mbili ambazo zitaanza kusikika siku chache zijazo.
Ukweli ni kuwa katiba mpya ya nchi ni lazima kwani kama kuna mabadiliko ya msingi ya kitaifa ni lazima pia katiba ibadilike. Kwa mfano wakati tunaingia katika mfumo wa vyama vingi na hata Tume ya Jaji Nyalali ilishauri katiba ibadilishwe, ikapuuzwa. Kunapokuwa na  mabadiliko kama vile kutoka kwenye utawala wa kikoloni kuja kwenye uhuru, lazima katiba ibadilike.
Hata wakati Afrika Kusini inapata uhuru kutoka serikali ya makaburu, ilikuwa lazima katiba ibadilishwe.
Mfano mwingine ni Rwanda baada ya kipindi chote cha mapambano na mauaji ya kutisha, ilihitajika kuwe na katiba mpya. Tumeona pia Sudan Kusini ambayo sasa imejitenga na Kaskazini ilihitajika katiba mpya.
Hata Kenya, walianza muda mrefu kudai katiba hadi nchi ilipoingia kwenye machafuko. Kwa hiyo hayo ni mabadiliko ya msingi ambayo yanalazimisha kuwepo kwa katiba mpya. Hali hiyo ya kuhitaji katiba mpya ipo hapa kwetu, wananchi wameonyesha kutoridhishwa na mambo mengi yanayoendelea nchini. Wanataka kuwe na mfumo mpya utakaoendesha nchi.
Kwa mfano, jambo kubwa linalolalamikiwa na kulazimisha kuwepo kwa Katiba Mpya ni uchaguzi.  Hili pia ni suala lililokuwa kwenye ushauri wa Tume ya Jaji Nyalali, likapuuzwa.  Alishauri iundwe tume huru ya uchaguzi, siyo kama hii ya sasa ambayo inateuliwa na rais ambaye pia ni mgombea kwenye uchaguzi.
Wananchi pia wanalalamikia kunyimwa haki ya mgombea binafsi, bunge la katiba limekataa licha ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kukubaliana hilo na mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba waliweka, ikang’olewa .
Mtu kama unataka kugombea ubunge au udiwani, ni lazima upitie kwenye chama. Sasa kwenye kampeni tutasikia kwa nini imeng’olewa na wanaopenda hilo akiwemo Mwenyekiti wa Democratic Party, Mchungaji Christopher Mtikila watasema kwa nini sheria hiyo iwepo.
Sijui kundi walilokataa hilo watawaambia nini wananchi Kumekuwa na sheria ya gharama za uchaguzi, lakini haitoi mwanya kwa vyama vidogo kuwa na matumizi makubwa kama vyama vikubwa.
Sheria hiyo haitekelezeki kwa sababu haijulikani inasimamiwa na nani. Ni Msajili wa Vyama vya Siasa au Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)?
Hata huyo, Msajili wa Vyama vya Siasa hana ofisi na watendaji nchi nzima, ataisimamiaje?
Kitu kingine ni mfumo mbovu wa sheria hiyo, kwa mfano Takukuru haieleweki ni jinsi gani itavishughulikia na vyama vingine kwa  sababu siyo kila chama kinafuata mfumo wa Chama Cha Mapinduzi.
Kwa kweli Takukuru hakuna wanalofanya kuhusu sheria hiyo. Wananchi wanalalamikia pia sheria ya kutopinga matokeo ya urais. Wanasema hii ni kasoro, kwa nini matokeo ya rais yasipingwe wakati wabunge na madiwani wanapingwa?
Wanasema hata Marekani wanapochagua rais wao kuna muda maalum umewekwa na katiba kabla ya kumwapisha, ili kama kuna dukuduku lolote litolewe. Wanalalamika hapa nyumbani, tume ikishamtangaza mtu, kesho yake anaapishwa, haraka ya nini?
Lakini nampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuunda  tume iliyokuwa inashughulikia katiba mpya japokuwa imemaliza vibaya kwa kubezwa na baadaye kuibuka makundi mawili ambayo yatapita kwetu kutuambia nini kizuri kipo na nini kibaya kimeondolewa.
Nchi hii ina maskini wengi na kiukweli wananchi wanajua chanzo cha umasikini wao, wanajua jinsi kulivyo na mfumo mbovu wa uongozi.Wananchi wanajiuliza kwa nini Tanzania ni maskini baada ya miaka 50 ya uhuru? Kwa nini umeme unasumbua? Wanasikia jinsi watu wanavyojilipa fedha nyingi kama vile kwenye sakata la Richmond, EPA, Dowans na Tegeta Escrow.
Wananchi watataka kusikia kwa wapiga debe wa katiba, nini kimo ndani ya katiba ambacho kitaziba mianya hiyo ya ufujaji wa fedha za umma. Pia watataka kujua kwa nini mbunge atawale jimbo kwa miaka 40 na kwa nini isiwe miaka 10 tu kama ilivyobadilishwa kwa rais?
Tutasikia kampeni za pande hizo mbili  na zisijidanganye kupindisha matakwa ya wananchi, kila upande usome alama za nyakati nasi raia tupime kila litakalosemwa.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Post a Comment

أحدث أقدم