Dar es Salaam. Miezi michache baada ya kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow kutikisa nchi, watumishi wawili waandamizi
wa Serikali wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam wakituhumiwa kupokea rushwa ya mamilioni ya fedha zilizotoka
kwenye akaunti hiyo.
Mahakama hiyo ilielezwa jana kuwa Mkurugenzi wa
Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Rugonzibwa Mujunangoma aliwekewa kiasi cha Sh323 milioni kupitia akaunti
yake namba 00120102602001.
Kadhalika, Mahakama ilielezwa kuwa Februari 12,
2014, Mhandisi Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (Rea), Wizara ya Nishati
na Madini, Theophillo Bwakea alipokea rushwa ya Sh161,700,000 kupitia
akaunti yake namba 004101102643901.
“Upelelezi wa kesi umekamilika naomba mahakama
izuie akaunti ya mshtakiwa iliyotumika kupokea fedha hizo za escrow na
kesi ipangwe kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali,” alisema Leonard
Swai ambaye ni Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru).
Akisoma hati ya mashtaka katika kesi namba 11 ya
mwaka 2015 inayomkabili Mujunangoma, Swai alidai mshtakiwa huyo alifanya
kosa hilo kinyume na kifungu cha 15 (1)cha Sheria ya Kupambana na
Rushwa, Namba 11 ya mwaka 2007.
Swai alidai kuwa Februari 5, 2014 katika Benki ya
Mkombozi iliyopo wilayani Ilala, Dar es Salaam, Mujunangoma akiwa
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa James Burchard
Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na
mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa
kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, Mujunangoma alikana
na mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru alidai kuwa kwa mujibu wa
kifungu cha 15 cha sheria anachoshtakiwa nacho, mshtakiwa huyo hahitaji
kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Emilius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo
kuwa na wadhamini wawili wanaofanya kazi katika taasisi ya Serikali na
kwamba kila mdhamini asaini hati ya maneno ya Sh10 milioni.
Pia, Hakimu Mchauru alimtaka mdhamini ama
mshtakiwa mwenyewe, kuwasilisha mahakamani hapo nusu ya fedha taslimu
anazodaiwa kuzichukua kama rushwa, ama kuwasilisha hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa masharti hayo,
mshtakiwa alipata wadhamini wawili wanaoaminika , kutoa hati mbili za
mali isiyohamishika ambazo alidai zina zaidi ya thamani ya fedha iliyomo
ndani ya hati ya mashtaka.
Kuhusu kuzuia akaunti ya mshtakiwa, Hakimu Mchauru
aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha maombi mahakamani hapo na
kuyaambatanisha na hati ya kiapo itakayounga mkono maombi hayo.
Kwa upande wa Bwakea, aliyefunguliwa kesi namba 12
ya 2015, Swai alidai kuwa siku hiyo ya tukio katika benki ya Mkombozi
alipokea rushwa ya kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti yake.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق