Dar es Salaam. Ni dhahiri mpambano wa kuwania
urais ndani ya CCM unazidi kunoga, ikiwa imebakia miezi michache kabla
ya kupulizwa rasmi kipenga.
Mmoja wa makada kutoka CCM waliotangaza nia ya
kuwania kiti hicho, January Makamba ameandikiwa kitabu kinachoeleza nia
yake hiyo.
Kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza
mikakati ya mwanasiasa huyo kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili
kuwania na hatimaye kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 196, Makamba
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mbunge
wa Bumbuli, Tanga anasema rais ajaye lazima awe na tafakuri pana na nia
ya kuendeleza nchi na siyo kuwa na kaulimbiu nyepesi za afya bure,
elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa wananchi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na mchambuzi na
mwandishi wa makala za siasa, Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na
mikakati yake kiundani ya kuiongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM
kugombea urais.
Katika kitabu hicho kinachoitwa, ‘Maswali na
Majibu 40: Mazungumzo na January Makamba kuhusu Tanzania Mpya’,
mwanasiasa huyo anasema uongozi hauishii kwa kauli za juu juu za
kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani kila mtu anaweza kuyasema hayo.
Anamwonaje rais ajaye
Anasema katika tafakuri zake anaona rais ajaye
anatakiwa kuzitambua kwa kina changamoto za nchi yake na kuwa na
mikakati ya kuzitatua.
Changamoto hizo, Makamba anasema ni za kiuongozi
na utatuzi wake unategemea kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na
usahihi wa uamuzi anaoufanya.
“Kuomba uongozi wa nchi siyo harakati binafsi na
wafuasi wako kupata vyeo. Ni dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa
nchi na kuwaunganisha Watanzania wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea
lazima uupe heshima na nafasi inayolingana na dhamana yenyewe,” anasema
Makamba kwenye kitabu hicho.
Anaongeza kuwa rais anatakiwa kuongeza kasi ya
kuondoa umaskini, kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali, vyombo vya
dola na mahakama na hayo yatadhihirika kwa vitendo vya kuchukua hatua
dhidi ya viongozi wabadhirifu, walarushwa na kudhibiti matumizi ya
Serikali.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق