Dar es Salaam. Chama cha ACT-Tanzania
kimewasimamisha viongozi wa chama hicho ambao ni Mwenyekiti wa muda
Kadawi Limbu na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Leopold Mahona na kikimvua
madaraka Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Grayson Nyakarungu.
Hatua hiyo imejitokeza baada ya maazimio ya
Halmashauri Kuu iliyokutana kujadili agenda za nidhamu ya mwenyekiti,
kupokea na kupitisha mwongozo na kanuni za uchaguzi pamoja ushiriki
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Katibu mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba
alisema jana kuwa maazimio ya mkutano huo yaliwachagua Shaaban Mambo
kuwa mwenyekiti wa muda, Mohamed Masaga, Naibu katibu mkuu na Hassan
Abdalah Omary kuwa mwenyekiti mpya wa vijana.
“Mkutano wa jana (juzi) ulikuwa na wajumbe 65,
lakini kura 57 zilipendekeza Limbu na Mahona wasimamishwe katika nafasi
zao kwa muda,” alisema Mwigamba na kuongeza kuwa: “Kwa mujibu wa katiba
ya chama, Kifungu cha 27(f) kinasema halmashauri ina mamlaka ya
kuwasimamisha kwa kipindi cha miezi sita, baada ya hapo watakuwa na haki
ya kugombea tena nafasi zao pindi uchaguzi utakapoitishwa.”
Alipoulizwa kuhusu uamuzi huo kama wameshawapatia na kuwajulisha wahusika, Mwigamba alisema tayari taratibu zote zilishafanyika.
“Kwanza tuliwapa nakala ya mashtaka pia tukawaita
kwenye mkutano ili kuwapatia nafasi ya kujitetea. Limbu alikataa
kujieleza,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, chama hicho kwa siku za hivi karibuni
kimekuwa katika mvutano kati ya Limbu na viongozi wenzake, hasa katibu
mkuu, akidaiwa kuhujumiwa na vyama vikubwa vya siasa.
Akizungumzia uamuzi huo, Limbu alisema siyo sahihi
kwani mkutano huo hauna mamlaka ya kumwondoa kwenye nafasi yake bali ni
kamati kuu tu ndiyo ina uwezo huo.
“Sheria ya vyama vya siasa ndiyo inatoa mamlaka.
Wajumbe waliokaa hatuna uhakika kama wamefikia akidi ya 65 kama
tulivyoelezwa,” alisema Limbu.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق