Dodoma. Usemi wa wahenga kuwa dalili ya mvua ni mawingu, una
mashiko na huonekana kufaa kwa watu wanaojiandaa kwa jambo fulani lililo
mbele yao.
Katika maandalizi ya mtu aliyedhamiria jambo huwa
si rahisi kukata tamaa hata kama atakumbwa na dhoruba za aina yoyote
lakini bado atahitaji kusonga mbele pasi kurudi nyuma.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo wasomi wengi
wamekuwa wakikimbilia katika siasa na kuziacha taaluma zao. Pengine ni
kutokana na kufuata masilahi na urahisi wa utendaji kazi.
Mbali na vijana, wapo wanaokimbia wakiwa kazini na
kuingia katika siasa. Miaka ya karibuni harakati zimekuwa zikianzia
vyuoni na baadhi ya walioshinda kwenye siasa tunashuhudia hadi sasa
wakiwa na nyadhifa mbalimbali Serikalini; wakiwemo mawaziri.
Mary Chacha (23) ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu
katika Chuo Kikuu cha St. John’s cha mjini Dodoma. Ni miongoni mwa
wasichana wenye ndoto ya kuwa wanasiasa wakubwa katika nchi.
Chacha anasoma Kitivo cha Elimu chuoni hapo ambaye
mbali na kuwaza kwenda kufundisha katika shule za vijijini; wanakoishi
watu wengi wa kipato cha chini, anatamani kupata nafasi ya uwakilishi wa
kisiasa hasa katika kofia ya ubunge ili awasemee watu wa vijijini.
Katika mazungumzo na Chacha ambaye hivi karibuni
alikuwa kinara wa uongozi kwa Bunge la Vijana, anasema kuwa ndoto ya
kuwa kiongozi alianza kuiwaza tangu akiwa shule ya msingi.
Bunge la Vijana liliandaliwa na Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuibua vipaji na kutoa fursa kwa
vijana, lilifanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa na Chacha aliteuliwa na
uongozi kushika nafasi ya Katibu. Bunge hilo lililosheheni vijana wa
vyuo vikuu nchini. Yafuatayo ni mahojiano na Chacha:
Hongera kwa kazi uliyoifanya ndani ya siku tatu mfululizo. Hebu tupe siri ya mafanikio yako katika kazi hii?
Jibu: Nashukuru kwa pongezi lakini nafasi hii ni
kwa neema ya Mungu ndiyo nimeweza kuliunganisha Bunge hili ambalo kwa
kweli ni gumu na lina changamoto nyingi za vijana.
Wakati unakuja katika bunge hili ulijua kwamba ungekuwa kiongozi au ilitokea baada ya kufika hapa ukumbuni?
Jibu. Ukweli nilikuja mimi kama mimi tena sikujua
kabisa kama nitakuwa hata na nafasi yoyote ingawa nilikuja nikiamini
nimejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kuwa mmoja wa wachangiaji wazuri.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق