Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga
na timu ya Taifa ya Tanzania, Edibily Lunyamila amezichambua Azam na
Yanga na kuzitaka ziondoe upungufu uliomo kwenye vikosi vyao kabla ya
kuanza kwa michuano ya Afrika baadaye mwaka huu.
Lunyamila ameitaka Azam ijiangalie upya kama
inataka kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwani kiwango
chake uwanjani kinatia shaka.
Alisema viungo wake washambuliaji wanatakiwa
kunolewa zaidi kama kweli wana nia ya kuitoa El- Merreikh ya Sudan
kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nao, Yanga ambao wameshinda mechi mbili zote kwa mabao 4-0, Lunyamila alisema wanatakiwa kujiangalia zaidi hasa ukuta na kipa.
“Yanga imeonekana iko moto katika michuano hiyo
huku ikiwa tishio kwenye upande wa ushambuliaji wakati Azam inasonga
mbele, lakini kiwango chake uwanjani hakiridhishi na kinatia shaka,”
alisema Lunyamila. Aliongeza kuwa amekuwa akifuatilia michuano ya
Mapinduzi na kueleza kuwa, Azam inatakiwa kujipanga kwani El- Mereikh
watakayokutana nayo si ya kubezwa hata kidogo.
“Azam wanatakiwa kujipanga kwani hata ukiangalia
kiwango chao kwenye michuano ya Mapinduzi hakivutii, wanacheza kawaida,
kocha wao (Joseph Omog) anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuitengeneza
timu yake.
“Tatizo Azam ni viungo, mechi zao zote
nilizoangalia viungo hawatengenezi nafasi za kufunga, muda mwingi
wanacheza pasi nyingi, lakini hazina maana kwa sababu hawapeleki mpira
mbele ili wafunge.”
Akiizungumzia Yanga, Lunyamila alisema timu hiyo
ina tatizo kubwa katika safu yao ya ulinzi hasa kipa, mabeki wa kati na
beki wa kushoto.
“Yanga inao viungo na washambuliaji wazuri, ila
tatizo kubwa kwenye ukuta wao, kwani licha ya kuwa wana mabeki wazoefu
na wanaoaminika kuwa bora hapa nchini, lakini wanafanya makosa.”
Post a Comment