Lunyamila azichambua Azam FC, Yanga SC

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Edibily Lunyamila amezichambua Azam na Yanga na kuzitaka ziondoe upungufu uliomo kwenye vikosi vyao kabla ya kuanza kwa michuano ya Afrika baadaye mwaka huu.
Lunyamila ameitaka Azam ijiangalie upya kama inataka kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwani kiwango chake uwanjani kinatia shaka.
Alisema viungo wake washambuliaji wanatakiwa kunolewa zaidi kama kweli wana nia ya kuitoa El- Merreikh ya Sudan kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nao, Yanga ambao wameshinda mechi mbili zote kwa mabao 4-0, Lunyamila alisema wanatakiwa kujiangalia zaidi hasa ukuta na kipa.
“Yanga imeonekana iko moto katika michuano hiyo huku ikiwa tishio kwenye upande wa ushambuliaji wakati Azam inasonga mbele, lakini kiwango chake uwanjani hakiridhishi na kinatia shaka,” alisema Lunyamila. Aliongeza kuwa amekuwa akifuatilia michuano ya Mapinduzi na kueleza kuwa, Azam inatakiwa kujipanga kwani El- Mereikh watakayokutana nayo si ya kubezwa hata kidogo.
“Azam wanatakiwa kujipanga kwani hata ukiangalia kiwango chao kwenye michuano ya Mapinduzi hakivutii, wanacheza kawaida, kocha wao (Joseph Omog) anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuitengeneza timu yake.
“Tatizo Azam ni viungo, mechi zao zote nilizoangalia viungo hawatengenezi nafasi za kufunga, muda mwingi wanacheza pasi nyingi, lakini hazina maana kwa sababu hawapeleki mpira mbele ili wafunge.”
Akiizungumzia Yanga, Lunyamila alisema timu hiyo ina tatizo kubwa katika safu yao ya ulinzi hasa kipa, mabeki wa kati na beki wa kushoto.
“Yanga inao viungo na washambuliaji wazuri, ila tatizo kubwa kwenye ukuta wao, kwani licha ya kuwa wana mabeki wazoefu na wanaoaminika kuwa bora hapa nchini, lakini wanafanya makosa.”

Post a Comment

أحدث أقدم