Kufunga mwaka na kufungua mwaka ni sikukuu zinazojirudia kila
mwaka. Kwa njia moja ama nyingine hakuna jinsi ya kukwepa kurudia maneno
yaleyale ya kila mwaka.
Imani yangu ni kwamba kuyarudia kila mwaka
kunaweza kutujengea utamaduni wa kuyatafakari matukio ya mwaka mzima na
kujipanga upya kwa mwaka unaoanza.
Mfano kushukuru na kuomba ni mambo ambayo lazima tuyarudie kila tunapofunga na kufungua mwaka.
Hivyo basi sote kwa pamoja tumshukuru Mwenyezi
Mungu, kwa kuuanza mwaka mpya wa 2015. Si kwa ubora wetu tumeendelea
kuishi, si kwa wema wetu tumeendelea kuishi na wala si kwa umuhimu wetu
tumeendelea kuishi.
Tunafahamu kabisa kwamba tuna watu wakatili
miongoni mwetu, lakini bado wanaendelea kuishi. Kuna watu wanatenda
maovu, wana chuki na roho ya kujilipiza kisasi, lakini bado wanaendelea
kuishi.
Tulikuwa na watu bora wenye wema wa kupindukia na
muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini hatunao tena!
Hawakubarikiwa kuiona 2015! Kuendelea kuwapo ni neema na huruma ya
Mwenyezi Mungu.
Hivyo kwa wale waliobahatika kuendelea kuishi ni
lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu. Mimi na wewe, kwa vile tunaishi,
tumshukuru Mwenyezi Mungu na kujitahidi kulijibu swali muhimu ambalo
nimekuwa nikilirudia mara kwa mara.
Swali la msingi la kujiuliza ni Je, kwa nini
Mungu, ameturuhusu kuendelea kuishi? Tunaishi ili tufanye nini? Tunaishi
ili tuendelee kula na kunywa? Tunaishi kufurahia maisha? Tunaishi ili
kuonyeshana ubabe?
Tunaishi ili kuwatesa wengine?
Tunaishi ili kuhakikisha tunayatumia madaraka yetu
kiubabe? Tunaishi kuhakikisha kwamba furaha tunayoipata sasa hivi
wajaliwe kuipata na wale wa vizazi vijavyo? Kwanini tuendelee kuwepo?
Pamoja na ukatili wetu na roho mbaya kwa nini Mungu anaendelea
kutulinda?
Je, Mungu anataka nini kutoka kwetu? Uhai
tunazawadiwa, hakuna anayeuomba! Lakini baada ya kuzawadiwa kila mwenye
uhai ana wajibu wa kuulinda.
- Mwananchi
- Mwananchi

إرسال تعليق