Dar es Salaam. Watanzania waliokuwa wakisubiri
kwa hamu kuanza kutumia umeme utokanao na mradi wa gesi asilia wa
Kinyerezi, sasa watahitajika kuvuta subira kidogo kutokana na uzalishaji
wa nishati hiyo kusogezwa hadi katikati ya mwezi ujao.
Awali, maofisa wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) na makandarasi wa mradi kwa nyakati tofauti,
walinukuliwa kuwa ujenzi ungekamilika Desemba mwaka jana na uzalishaji
wa majaribio ungeanza mapema mwezi huu.
Hata hivyo, ripoti ya maendeleo ya mradi huo
iliyotolewa jana na TPDC inaonyesha kuwa baadhi ya masuala ya ujenzi na
ununuzi yanatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na Februari.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ujenzi wa mradi mzima
wa bomba hilo la gesi linalotokea Mtwara hadi Kinyerezi, ulikuwa
umekamilika kwa asilimia 94.8 wakati ununuzi ulikuwa ni asilimia 99
mwishoni mwa Novemba.
Akielezea kilichochelewesha, Meneja wa mradi huo
kutoka TPDC, Kapuulya Musomba alisema kuwa uzalishaji wa majaribio
umesogezwa kutokana na tatizo la usafirishaji wa vifaa lililoathiri
ratiba ya awali. Uzalishaji rasmi unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu.
“Kuna wakati tulikuwa tukitegemea mitambo
iliyoingia bandarini ingetolewa ndani ya wiki moja, lakini haikuwa
hivyo,” alisema Musomba.
Kuhusu uwapo wa uchakachuaji wa kuongeza bei mara
mbili ya mradi huo, Musomba alisema kiasi cha Sh2 trilioni walizoomba
kukamilisha ujenzi huo ndizo zilizomo kwenye mkataba. Novemba, 2014
akiwa mjini Nzega, mkoani Tabora, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
aliwatuhumu vigogo wa Serikali kwa ufisadi wa kuongeza Dola 600 milioni
za Marekani (Sh1.02 trilioni) katika ujenzi wa mradi huo hali iliyofanya
gharama ziongezeke mara mbili na kufikia Sh2.4 trilioni.
Alisema kuwa awali kampuni inayojenga bomba hilo,
ilisema gharama halisi za mradi huo ilikuwa Sh1.20 trilioni, lakini wao
wakaongeza mara mbili ya fedha hizo kwa manufaa yao binafsi.
Msomba alibainisha kuwa TPDC haishiriki kumlipa
moja kwa moja Mkandarasi zaidi ya kukagua madai ya mkandarasi huyo,
kuishauri serikali iidhinishe na hatimaye mkopeshaji wa mradi, Exim Bank
ndiye ambaye hulipa fedha hizo moja kwa moja.
“Hata ukiangalia kwenye riba bado mkopo wetu una
malipo ya chini sana kuwahi kutokea. Asilimia 75 ya mkopo huo ina riba
ya asilimia mbili wakati zilizobakia zina riba ya asilimia 4.3 hivi ni
benki gani ulimwenguni inaweza kukopesha kwa kiasi hicho?,” alihoji
Mhandisi huyo.
Alisema hana nguvu ya kubishana majukwani na
wanasiasa juu ya gharama halisi za mradi huo lakini anayetaka
kujiridhisha afanye uchunguzi na kufanananisha na uhalisia wa gharama za
ripoti hiyo.
Sehemu hiyo ya kwanza ya mradi wa megawati 150
inajengwa na Shirika la Teknolojia ya Petroli na Maendeleo la China
(CPTDC) kwa ushirika na kampuni ya Jacobsen Elektro AS ya Norway.

إرسال تعليق