Tuzidi kuijenga Tanzania yetu kwa amani na usalama

Kufunga mwaka na kufungua mwaka ni sikukuu zinazojirudia kila mwaka. Kwa njia moja ama nyingine hakuna jinsi ya kukwepa kurudia maneno yaleyale ya kila mwaka.
Imani yangu ni kwamba kuyarudia kila mwaka kunaweza kutujengea utamaduni wa kuyatafakari matukio ya mwaka mzima na kujipanga upya kwa mwaka unaoanza.
Mfano kushukuru na kuomba ni mambo ambayo lazima tuyarudie kila tunapofunga na kufungua mwaka.
Hivyo basi sote kwa pamoja tumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuuanza mwaka mpya wa 2015. Si kwa ubora wetu tumeendelea kuishi, si kwa wema wetu tumeendelea kuishi na wala si kwa umuhimu wetu tumeendelea kuishi.
Tunafahamu kabisa kwamba tuna watu wakatili miongoni mwetu, lakini bado wanaendelea kuishi. Kuna watu wanatenda maovu, wana chuki na roho ya kujilipiza kisasi, lakini bado wanaendelea kuishi.
Tulikuwa na watu bora wenye wema wa kupindukia na muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini hatunao tena! Hawakubarikiwa kuiona 2015! Kuendelea kuwapo ni neema na huruma ya Mwenyezi Mungu.
Hivyo kwa wale waliobahatika kuendelea kuishi ni lazima kumshukuru Mwenyezi Mungu. Mimi na wewe, kwa vile tunaishi, tumshukuru Mwenyezi Mungu na kujitahidi kulijibu swali muhimu ambalo nimekuwa nikilirudia mara kwa mara.
Swali la msingi la kujiuliza ni Je, kwa nini Mungu, ameturuhusu kuendelea kuishi? Tunaishi ili tufanye nini? Tunaishi ili tuendelee kula na kunywa? Tunaishi kufurahia maisha? Tunaishi ili kuonyeshana ubabe?
Tunaishi ili kuwatesa wengine?
Tunaishi ili kuhakikisha tunayatumia madaraka yetu kiubabe? Tunaishi kuhakikisha kwamba furaha tunayoipata sasa hivi wajaliwe kuipata na wale wa vizazi vijavyo? Kwanini tuendelee kuwepo? Pamoja na ukatili wetu na roho mbaya kwa nini Mungu anaendelea kutulinda?
Je, Mungu anataka nini kutoka kwetu? Uhai tunazawadiwa, hakuna anayeuomba! Lakini baada ya kuzawadiwa kila mwenye uhai ana wajibu wa kuulinda.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post