Kuna hatari ya kuenea chuki dhidi ya raia wa kigeni Ujerumani.
Hisia dhidi ya Uislamu zimezidi siku hizi katika nchi hiyo. Kumekuwa
kukiripotiwa matukio ya kushambuliwa misikiti na makazi ya wahamiaji.
Visa hivyo vinatokana na kuundwa kwa vuguvugu lenye jina la PEGIDA,
yaani Wazalendo wa Ulaya wanaopinga kuenea Uislamu katika nchi za
Magharibi. Kundi hilo lilianzia mjini Dresden likiwa lina watu 300,
lakini sasa linajivunia wanachama wanaokaribia 20,000 nchini Ujerumani.
Kundi hilo hufanya maandamano kila Jumatatu katika miji tofauti huku
likiwa limebeba mabango yenye maandishi ya chuki dhidi ya raia wa kigeni
na pia kuupinga Uislamu. Visa vya kuwachukia raia wa kigeni vimekuwa
vikizidi, hali inayoashiria kwamba wananchi wa Ulaya wanazidi kuelemea
katika siasa za mrengo wa kulia. Mambo yalikuwa kama hivi; raia wa
Norway, Anders Behring Breivik, alipofanya mauaji mjini Oslo mwaka 2011,
kwanza alilipua bomu mbele ya majengo ya Serikali na baadaye
akaishambulia kambi ya tawi la vijana ya chama tawala cha Labour. Aliua
watu 77, akidai kwamba amefanya hivyo kutokana na msimamo wake dhidi ya
Uislamu, pia kupinga kuweko mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali nchini
Norway.
Chuki
Chuki dhidi ya raia wa kigeni huchochewa na
wanasiasa. Kwa mfano, chama cha mrengo wa kulia nchini Ufaransa ambacho
sasa kinaongozwa na Marine Le Pen kilikuwa ni chama kidogo katika miaka
ya themanini na kilikuwa kati ya vyama vya mwanzo kuushutumu Uislamu na
kutaka raia wa kigeni warejeshwe makwao.
Hivi sasa Bibi Le Pen ni mtetezi ambaye huenda akaongoza katika uchaguzi wa urais mwaka 2017.
Siasa dhidi ya Uislamu na kuwachukia wageni ni
bidhaa inayouzwa kwa urahisi hivi sasa na wanasiasa wa mrengo wa kulia
sana katika nchi kadhaa za Ulaya.
Kweli, usasa na utandawazi umeharakisha kuja kwa
mabadiliko ya kijamii tunayoyaona na ambayo pia yanasababishwa na idadi
kubwa ya watu wanaohama kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Hali hiyo inasababisha kuwako na hofu miongoni mwa
watu wa nchi yeyote kwamba huenda wakapoteza utambulisho wao na kile
walicho nacho.
Ni kawaida kwamba inajengeka chuki pale panapokuwako kundi la watu walio nacho na kundi jingine la watu wasiokuwa nacho.
Iko hofu kwamba maelfu ya wakimbizi kutoka
Mashariki ya Kati na Afrika, wanaovuka Bahari ya Mediterania, wanaingia
Ulaya kuwapokonya au kuwapunguzia wazawa wa Ulaya neema walio nayo.
Hivyo, inafaa wazuiwe, pia bahari hiyo ya Mediteranea igeuzwe kuwa ukuta usiopitika baina ya Afrika na Ulaya.
Nchi nyingi za Ulaya zina neema, hasa Ujerumani,
ukilinganisha na nchi nyingi nyingine nje ya bara hilo. Wazawa wa nchi
za Ulaya hujisifu kwamba neema yao inatokana na mfumo wao wa utawala wa
demokrasia na usasa.
Post a Comment