Watu wengi hawajui kuwa kupitia simu yako ya mkononi, tabiti, au
kompyuta yenye mtandao, unaweza kununua bidhaa zako na kuzipata kwa
muda mfupi mlangoni kwako.
Kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (Tehama) imefungua milango ya kununua bidhaa mtandaoni kwa
kuyavuta maduka na kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa kwa kuonana na
muuzaji.
Kampuni kadhaa za nje na za ndani kama Kaymu,
Hellofood, Kivuko, Jumuia, ShoppingTz na nyinginezo, zimeanzisha huduma
hiyo ili kutumia fursa adhimu ya biashara katika jamvi la Tehama.
Biashara hii inafanyikaje?
Katika soko au duka la mtandaoni, mteja na muuzaji
hawakutani ana kwa ana, bali kupitia mtandao kwa kuunganishwa kupitia
tovuti au programu ya simu (‘app’) ambazo nyingi humilikiwa na kampuni
za kijasiriamali.
Tovuti hizo huwa ni jamvi au meza ambazo wauzaji
huweka taarifa zao za kina kama vile bei na aina ya bidhaa, idadi,
kiwango, mwaka wa kutengenezwa (kwa bidhaa za kuisha muda) na uwezo
wake.
Taarifa hizo huambatana na picha halisi za bidhaa
ili kuzuia utata unaoweza kutokea mteja anapokuta bidhaa aliyonunua na
kuletewa siyo ile iliyopo pichani. Programu ya kompyuta inayofanya kazi
kama kikapu hutumika kufanikisha ununuzi kwa kumjulisha mnunuzi jumla ya
bidhaa alizonunua na fedha anazodaiwa.
Katika tovuti hizo kuna kila aina ya bidhaa
kuanzia nguo, vyakula, magari, vitabu, vifaa vya elektroniki, vipodozi,
vidani, muziki, video na vinginevyo.
Malipo
Malipo katika biashara hiyo iliyoanzishwa miaka 35
iliyopita na mjasiriamali Mwingereza Michael Aldrich, yanaweza
kufanyika moja kwa moja mtandaoni au wakati mteja anapopokea bidhaa.
Meneja Mkuu wa kampuni ya kuuza chakula mtandaoni,
Sherrian Abdul anasema wateja wanaweza kulipia kupitia Tigo Pesa (kwa
sasa) au kulipia wakati wanapokea chakula.
Pia, shoponlinetz kupitia tovuti yao wamebainisha
kuwa wateja wanaweza kufanya malipo yao kupitia kampuni za malipo za
Visa, Visa Electron, Paypal, Mastercard, Airtel Money na Tigo pesa.

إرسال تعليق