Majambazi Yavamia Duka la M-Pesa na Kupora Milioni 45

MAJAMBAZI watano wakiwa na silaha za moto na mapanga wamevamia duka la fedha la Mji mdogo wa Sirari na kupora Sh milioni 45 za Kitanzania na fedha za Kenya elfu 50.
 
Katika hekaheka hizo majambazi hao wamejeruhi watu wawili akiwemo mwalimu wa shule ya msingi Sirari anayeitwa Mataigwa Muhono (30) aliyepigwa risasi mguuni na mdogo wa mwenye duka ambaye alikuwa akitoa huduma Mara Masabi (23) ambaye amepigwa mapanga. Duka hilo mali ya Dickson Ntari (32) lipo hatua 20 kutoka kizuizi cha kituo cha Forodha Sirari.
 
Aidha majambazi hao baada ya kumaliza uvamizi katika duka la Dickson walivamia na maduka jirani kabla ya kukimbilia nchi jirani ya Kenya. Kaimu Kamanda wa mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya, Sweetbart Njewike alikiri kutokea kwa tukio hilo Alhamisi jioni ya Januari 15 mwaka huu.
 
Alisema kwamba majambazi hao wakiwa na makoti meusi na mmoja aliyebeba bunduki ya vita aina ya AK 47 akiwa katika koti jekundu alipiga risasi hewani kudhibiti watu waliokuwa wanataka kutoa msaada na ndipo alipomjeruhi mwalimu huyo.
 
Pamoja na kupora fedha taslimu Sh za kitanzania 40 ,000,000 katika duka la Dickson pia walipora simu za mkononi 3 aina ya Samsung zenye thamani ya Sh 850,000, simu 3 aina ya Nokia zenye thamani ya Sh 290,000.
 
Aidha kwenye duka jirani linalomilikiwa na Charles Papa Nestory walipora Sh 350,000 na fedha za Kenya 50,000 wakati mfanyabiashara anayemiliki jengo la Wazee Sirari anayetambulika kwa jina la Elisha Kaduri aliporwa 2,700,000 alizokuwa amelipwa kodi ya nyumba.
 
Kaimu Kamanda huyo ACP Sweetbat Njewike alisema majambazi hao walikimbia baada ya kuona kwamba wanaanza kuzidiwa na wafanyabiashara wengine waliokuwa na silaha ambao walijitokeza kukabiliana nao kabla ya polisi kufika.
 
Hata hivyo alisema kwamba majambazi hao walifanikiwa kutoroka na kutokomea porini njia ya kuelekea mji wa Isebania. Hili ni tukio la sita la majambazi kuvamia na kupora watu fedha katika maeneo hayo ya maduka.
 
Katika moja ya matukio hayo kaka mkubwa wa Dickson Ntari aitwaye Mwita Ntari aliwahi kuvamiwa na kuporwa zaidi ya Sh milioni 60 na watu waliokuwa na silaha za moto.
 
Aidha wameshawahi kuvamia baa ya ya Mzalendo mali ya Ikonde Mrimi na kuwaua wateja wawili akiwemo raia wa Kenya na fundi ujenzi.

Post a Comment

أحدث أقدم