Katikati ya wiki hii nilikuwa mmoja wa waandishi wa habari
waliohudhuria kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(Laac), ambayo ilikutana na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo ilikutana na watendaji hao kwa ajili
ya kupata maelezo ya kina baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha wa 2012/13, kuonyesha kuwa
Halmashauri hiyo ina matatizo makubwa katika matumizi ya fedha na
kuingia mikataba mibovu.
Katika kikao hicho Laac iliibua ‘madudu’
yanayoonyesha jinsi watendaji wa halmashauri hiyo walivyotafuna fedha za
miradi na kuingia mikataba ya kifisadi jambo lililosababisha zaidi ya
Sh2 bilioni kutojulikana zilipo.
Madudu hayo yaliyosababisha kamati hiyo kushindwa
kukagua miradi ya maendeleo na kuhoji mambo mengine, kuipa Halmashauri
hiyo muda wa wiki mbili iwe imepata nyaraka zote zinazoonyesha fedha za
miradi zilivyotumika pamoja na mikataba yote.
Kwa jinsi Mkaguzi Msaidizi wa Hesabu za Serikali,
Emmanuel Kalibashubao alivyokuwa akieleza masuala ya mikataba, miradi ya
Halmashauri hiyo iliyopo katika ripoti ya CAG, ilinifanya nilikumbuke
kundi la vijana la Panya Road.
Kundi hilo limekuwa tishio jijini Dar es Salaam
kwani huvamia watu na kuwapora, hata wananchi wanapopewa taarifa kuwa
vijana hao wako maeneo ya karibu (hata kama si kweli), hushikwa na
mchecheto na kukimbia ovyo ili kuwakwepa.
Nalifananisha kundi hilo na yaliyoibuliwa na Laac
kwa sababu ndani ya Halmashauri ya Kinondoni kuna baadhi ya watendaji
wana tabia kama za kundi hili.
Wakati ‘Panya Road’ ninaowafahamu mimi wakivamia
watu mitaani na kuwapora fedha, Panya Road hawa wa Halmashauri ya
Kinondoni ambao ni baadhi tu ya watendaji, wanatafuna fedha za umma bila
jasho, bila kuwatisha wananchi na hakuna polisi anayewasaka ili
kuwakamata.
Katika ripoti ya CAG inaonyesha kati ya miradi 15 ya Halmashauri hiyo, 11 mahesabu yake yahaeleweki na hayapo sahihi.
Kati ya miradi hiyo, mmoja ni wa Sh4 bilioni lakini ilibainishwa kuwa Sh1 bilioni haijulikani ilipo.
Hata Laac ilipomtaka mkaguzi wa ndani wa Manispaa
hiyo kutoa majibu ya miradi hiyo, hakuweza kujibu chochote na jambo la
kushangaza ni kwamba CAG alikutana na watendaji wa Manispaa hiyo mara
tatu lakini walishindwa kurekebisha kasoro hiyo.
Jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya mikataba
ya uwekezaji katika Halmashauri hiyo, ukiwemo wa Oysterbay Villa
ilifichwa na hata CAG alipoitaka kwa ajili ya kufanya ukaguzi alinyimwa
na watendaji wa manispaa hiyo. Katika majibu yake, Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Mussa Natty aliijibu Laac kuwa anayetakiwa kujibu maswali
ya mkataba huo ni Mussa Masanja ambaye alikuwa Ofisa Manunuzi wa
Manispaa hiyo kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Katiba na Sheria.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق