Mapya yaibuka vurugu za Panya Road

Dar es Salaam. Baada ya saa 24 kupita tangu kundi maarufu la waporaji la Panya Road, kuvamia na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, chanzo cha uhalifu huo kimebainika.
Hali hiyo iliwafanya wakazi wa jiji hilo kusitisha shughuli mbalimbali kutokana na kuhofia usalama wao, huku usafiri ukiadimika.
Tukio hilo linaelezwa lilitokea ikiwa ni ishara ya kundi hilo kumuenzi mwenzao aliyefikwa na mauti akidaiwa kutaka kuiba pikipiki.
Mkazi wa Magomeni Kagera, Mohamed Chalamira alisema, “Wakati wakitoka kuzika walikuwa wakiambiana kuwa mwanajeshi hawezi kuuawa na kuzikwa bila kupigwa mizinga hivyo tutakwenda kulianzisha ili polisi wapige mabomu na ndicho kilichotokea.”
Aliongeza: “Ni tukio lililotuacha tukishangaa, kwani polisi mmoja aliyekuwa na silaha alitaka kumkamata mwenzao, lakini alipotoa panga tu yule polisi alikimbia, hii haiwezekani yaani polisi anakimbia mhalifu? Ilikuwa saa 9 vijana waligeuza eneo hilo (Magomeni Kagera) kama eneo lao.”
Kuhusu vijana waliokamatwa Chalamira alisema: “Hao vijana wawili waliokamatwa mmoja kweli anahusika, lakini mwingine ni hahusiki kwani dereva, huyo mshikaji atasota huko wakati hahusiki, polisi wafanye uchunguzi wao kwani haiwezekani kundi hili likasababisha mtafaruku...Mimi mwenyewe juzi nimepoteza simu na nimeumia hapa katika goti.”
Familia yazungumza
Kaka mkubwa wa marehemu, Mohamed Ayubu maarufu ‘Diamond’, Moshi Hamadi alisema mdogo wake huyo alizaliwa mwaka 1995 Magomeni Kagera na kukulia  kwenye familia hiyo, lakini aliondoka kutokana na tabia zake kuanzia kubadilika.
Alisema Ayubu hakubahatika kumaliza elimu ya msingi kutokana na kujiingiza katika makundi ya wavuta bangi akiwa darasa la nne na alipoonywa hakukubali na alichukia na kuamua kuondoka nyumbani kwao.
“Huyu alikuwa ni mtoto wa pekee kwa mama yake, hakuwahi kupata mtoto mwingine, ndiyo maana hawezi kuzungumza presha imempanda,” alisema Hamad baada ya mwandishi kuomba kuzungumza na mama yake mzazi na alijibiwa hivyo.
Kauli ya Hamadi iliungwa mkono na mama mkubwa wa marehemu Ndam Moshi ambaye alisema Ayubu hakutaka vitendo vyake vijulikane na alipokuwa akienda kuwasalimia walipomgusia kwamba siku hizi anajihusisha na masuala ya wizi alikuwa anakataa na kulia kutwa nzima.
Kuhusu taarifa za kifo chake, Hamadi alisema walipigiwa simu na vijana wasiowafahamu kuwataarifu kuwa Diamond amefariki dunia kwa kukatwa mapanga eneo la Tandale kwa Mtogole ambako kulikuwa na mkesha wa Mwaka Mpya

Post a Comment

أحدث أقدم