Makalio ya sufuria hayaogopi moto; mchana inzi na usiku mbu;
mawifi liwe liwalo tutaolewa tu na kaka zenu. Mpo hapo? Basi kero za
nini na mlikuwa wapi wakati kaka zenu walipotutafuta, kutupenda hatimaye
kutuoa? Mwakwetu, hilo ni tamko la Jamila kwao ‘mawifi’ wakorofi.
Wifi ni tamko linalotumiwa au wanaloitana baina ya
mke na ndugu wa kike wa mume. Yasemekana ati ‘mawifi’ wengi hasa wale
ndugu wa mume haswa huwa na ukorofi usio na tija kwa wake wa kaka zao na
jambo hili hutokea zaidi baada ya kaka zao kuoa na siyo sana wakati wa
‘uchumba’ wao.
Binti Kibena anazoza hivi ‘…Wifi mbona sikuelewi
ugomvi na vijineno-neno visivyokwisha vya nini, kama vile twagombea mume
ilhali huyu ni kaka yako, husuda ya nini? Naye Johari anamwambia dada
wa mumewe ‘…Mwenzangu elewa kaka yako kanichagua mie, keshaniweka ndani
kwa mahari tosha na ‘mkaja’ wa mama kautoa; wewe waipaza roho yako juu
kama moto wa kifuu cha nazi kwa lipi? Heheee utaidhili nafsi yako
mwenyewe.
Kero na mashaka
Ijapokuwa siyo kawaida ndani ya jamii kulitegemea
jambo hili kutokea yaani kwa mawifi kutoelewana bado huwa linatamkwa
kama angalizo kwa wake wengi wa makaka au waume wenye madada. Nasema
hivyo pia ieleweke yakuwa ‘kutoelewana’ baina ya mawifi siyo jambo au
tukio la upande mmoja.
Wapo baadhi ya wake ambao nao huzusha kero kubwa
kwa wanandugu wa waume zao, wengine lengo lao ni kutaka kumshika
kisawa-sawa au kumdhibiti mume wake asisikie lolote kutoka kwa nduguze
na wengine huwa na hulka na husuda mbaya tu. Pia, hata wengine ambao
hujihami kwa kumtenga mume na ndugu zake kutokana na kasoro au udhaifu
wao wa maisha walionao.
Zipo sababu za mashaka zinazowazingira baadhi ya
wake-mawifi, wengine hapo awali huko watokako wamekuwa wakiishi maisha
ya ‘ukahaba’ hadi walipokutana na jamaa ambaye ameamua kufunga ndoa
naye. Wana mashaka na kujitahidi kuiweka siri ya maisha ya awali. Wapo
ambao waliolewa awali na kuachika na wapo ambao wamekuwa na tabia chafu
ya kutoa mimba mara kadhaa nao wanahofia pengine kutokuwa na uwezo tena
wakushika mimba kikamilifu na kuzaa. Wengine ni hitilafu na udhaifu wa
viungo vya uzazi-ni kawaida hutokea. Ni mashaka tu.
Hivyo basi, wake-mawifi huwa na tabia kali ya kujihami na kukosa ‘kujiamini’.
Mke ambaye amezingirwa na hali hiyo huishi katika
wimbi la mashaka makubwa na niwe muwazi, huyu huhatarisha maisha yake
mwenyewe kwani anakuwa na ‘msongo wa mawazo’ wakati wote, yaani pia ni
hatari kwa maisha mema na endelevu kwa wanajamii wanaomzunguka na kuhisi
kuonewa tu wakati wote; huishia kuamua kujitenga na ndugu wa mumewe
hasa mawifi zake.
Wapo baadhi ya ‘wake’-mawifi ambao kutokana na
mashaka yao wenyewe hujifanya kuwa wacha Mungu na kujiita ‘wameokoka’ au
wao ni ‘wa-swala tano’ lakini tabia zao siyo nzuri asilani na hata
kuwahisi vibaya ndugu wakaribu wa waume zao; wengine wanagubikwa na
vitendo viovu vya utesaji wa watoto kisaikolojia hawa hawako karibu na
Mwenyezi Mungu ni unafiki tu.
Dada wa mume-wifi
Baadhi ya dada nao wamekuwa na tabia ya utegemezi
kwa kaka zao kabla hawajaoa, hivyo basi hujijengea hofu ya kwamba pindi
kaka zao wanapooa basi watakosa uhuru waliokuwa nao kwao; kukosa
mahitaji yao-kifedha hatimaye kwa upumbavu tu watu wa mjini husema
‘…Wanawajengea bifu mawifi zao’. Ni ujinga tu.
Post a Comment