Mawifi pande zote mpendane

Makalio ya sufuria hayaogopi moto; mchana inzi na usiku mbu; mawifi liwe liwalo tutaolewa tu na kaka zenu. Mpo hapo? Basi kero za nini na mlikuwa wapi wakati kaka zenu walipotutafuta, kutupenda hatimaye kutuoa? Mwakwetu, hilo ni tamko la Jamila kwao ‘mawifi’ wakorofi.
Wifi ni tamko linalotumiwa au wanaloitana baina ya mke na ndugu wa kike wa mume. Yasemekana ati ‘mawifi’ wengi hasa wale ndugu wa mume haswa huwa na ukorofi usio na tija kwa wake wa kaka zao na jambo hili hutokea zaidi baada ya kaka zao kuoa na siyo sana wakati wa ‘uchumba’ wao.
Binti Kibena anazoza hivi ‘…Wifi mbona sikuelewi ugomvi na vijineno-neno visivyokwisha vya nini, kama vile twagombea mume ilhali huyu ni kaka yako, husuda ya nini? Naye Johari anamwambia dada wa mumewe ‘…Mwenzangu elewa kaka yako kanichagua mie, keshaniweka ndani kwa mahari tosha na ‘mkaja’ wa mama kautoa; wewe waipaza roho yako juu kama moto wa kifuu cha nazi kwa lipi? Heheee utaidhili nafsi yako mwenyewe.
Kero na mashaka
Ijapokuwa siyo kawaida ndani ya jamii kulitegemea jambo hili kutokea yaani kwa mawifi kutoelewana bado huwa linatamkwa kama angalizo kwa wake wengi wa makaka au waume wenye madada. Nasema hivyo pia ieleweke yakuwa ‘kutoelewana’ baina ya mawifi siyo jambo au tukio la upande mmoja.
Wapo baadhi ya wake ambao nao huzusha kero kubwa kwa wanandugu wa waume zao, wengine lengo lao ni kutaka kumshika kisawa-sawa au kumdhibiti mume wake asisikie lolote kutoka kwa nduguze na wengine huwa na hulka na husuda mbaya tu. Pia, hata wengine ambao hujihami kwa kumtenga mume na ndugu zake kutokana na kasoro au udhaifu wao wa maisha walionao.
Zipo sababu za mashaka zinazowazingira baadhi ya wake-mawifi, wengine hapo awali huko watokako wamekuwa wakiishi maisha ya ‘ukahaba’ hadi walipokutana na jamaa ambaye ameamua kufunga ndoa naye. Wana mashaka na kujitahidi kuiweka siri ya maisha ya awali. Wapo ambao waliolewa awali na kuachika na wapo ambao wamekuwa na tabia chafu ya kutoa mimba mara kadhaa nao wanahofia pengine kutokuwa na uwezo tena wakushika mimba kikamilifu na kuzaa. Wengine ni hitilafu na udhaifu wa viungo vya uzazi-ni kawaida hutokea. Ni mashaka tu.
Hivyo basi, wake-mawifi huwa na tabia kali ya kujihami na kukosa ‘kujiamini’.
Mke ambaye amezingirwa na hali hiyo huishi katika wimbi la mashaka makubwa na niwe muwazi, huyu huhatarisha maisha yake mwenyewe kwani anakuwa na ‘msongo wa mawazo’ wakati wote, yaani pia ni hatari kwa maisha mema na endelevu kwa wanajamii wanaomzunguka na kuhisi kuonewa tu wakati wote; huishia kuamua kujitenga na ndugu wa mumewe hasa mawifi zake.
Wapo baadhi ya ‘wake’-mawifi ambao kutokana na mashaka yao wenyewe hujifanya kuwa wacha Mungu na kujiita ‘wameokoka’ au wao ni ‘wa-swala tano’ lakini tabia zao siyo nzuri asilani na hata kuwahisi vibaya ndugu wakaribu wa waume zao; wengine wanagubikwa na vitendo viovu vya utesaji wa watoto kisaikolojia hawa hawako karibu na Mwenyezi Mungu ni unafiki tu.
Dada wa mume-wifi
Baadhi ya dada nao wamekuwa na tabia ya utegemezi kwa kaka zao kabla hawajaoa, hivyo basi hujijengea hofu ya kwamba pindi kaka zao wanapooa basi watakosa uhuru waliokuwa nao kwao; kukosa mahitaji yao-kifedha hatimaye kwa upumbavu tu watu wa mjini husema ‘…Wanawajengea bifu mawifi zao’. Ni ujinga tu.

Post a Comment

أحدث أقدم