Ni zaidi ya miaka 20 sasa imepita bila mgogoro wa ardhi katika
eneo la Pori Tengefu la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mgogoro huu ambao awali ulikuwa kati ya mwekezaji
wa uwindaji wa kitalii kutoka Falme za Kiarabu na wananchi wa vijiji
sita vinavyozunguka eneo hilo, sasa umepanuka na kuihusisha Serikali na
mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs.
Mwanzoni mwa miaka ya 90, Kampuni ya Ortelo
Business Cooperation (OBC), inayomilikiwa na familia ya Kifalme iliingia
mkataba wa uwekezaji (uwindaji wa kitalii) na Serikali kupitia
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya wananchi.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro enzi hizo,
Richard Koila alisaini kwa niaba ya wananchi kuruhusu OBC kuwinda ndani
ya maeneo ya vijiji kwa makubaliano ya kuchangia gharama za miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, elimu na miundombinu.
Pamoja na upinzani mkali kutoka kwa wananchi, OBC
iliendelea kuwepo na bado ipo huku ikitekeleza baadhi ya makubaliano
yaliyo ndani na nje ya mkataba.
Kampuni hiyo imejenga shule ya sekondari na nyumba ya kupumzikia wageni mashuhuri katika eneo la Wasso.
OBC imeshiriki na inaendelea kulipia gharama za
elimu kwa watoto kutoka jamii ya kifugaji ya Maasai kuanzia shule ya
msingi, sekondari hadi vyuo kikuu.
Inadaiwa kuwa hata baadhi ya vijana wa Kimaasai
wanaoongoza mapambano ya kuipiga vita kampuni hiyo kupitia NGO
walizozianzisha baada ya kuhitimu masomo, wamesomeshwa aidha kwa gharama
zote za elimu yao au sehemu kulipiwa na OBC.
Kampuni hiyo imechimba visima vya maji katika
maeneo mbalimbali Loliondo, ingawa nakiri kutojua uhakika wa upatikanaji
wa maji katika visima hivyo.
Miaka ya tisini, OBC ilitoa mabasi kwa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Loliondo.
Licha ya madai ya mabasi hayo kuhitaji gharama
kubwa ya uendeshaji ikiwemo matumizi makubwa ya mafuta na vipuri, lakini
yalipokelewa, kutumiwa na hatimaye kuwekwa juu ya mawe baada ya kampuni
kuacha uendeshaji mikononi mwa halmashauri.
Nimeeleza kwa kirefu baadhi ya mambo, yaliyotendwa
na OBC ili kujenga hoja ninayolenga kuijadili ambayo ni kwanini
wananchi wa Loliondo wameendelea kupiga vita OBC kwa miaka zaidi ya 20
sasa.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق