Miaka 20 mgogoro wa ardhi Loliondo imetosha

Ni zaidi ya miaka 20 sasa imepita bila mgogoro wa ardhi katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mgogoro huu ambao awali ulikuwa kati ya mwekezaji wa uwindaji wa kitalii kutoka Falme za Kiarabu na wananchi wa vijiji sita vinavyozunguka eneo hilo, sasa umepanuka na kuihusisha Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs.
Mwanzoni mwa miaka ya 90, Kampuni ya Ortelo Business Cooperation (OBC), inayomilikiwa na familia ya Kifalme iliingia mkataba wa uwekezaji (uwindaji wa kitalii) na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya wananchi.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro enzi hizo, Richard Koila alisaini kwa niaba ya wananchi kuruhusu OBC kuwinda ndani ya maeneo ya vijiji kwa makubaliano ya kuchangia gharama za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji, elimu na miundombinu.
Pamoja na upinzani mkali kutoka kwa wananchi, OBC iliendelea kuwepo na bado ipo huku ikitekeleza baadhi ya makubaliano yaliyo ndani na nje ya mkataba.
Kampuni hiyo imejenga shule ya sekondari na nyumba ya kupumzikia wageni mashuhuri katika eneo la Wasso.
OBC imeshiriki na inaendelea kulipia gharama za elimu kwa watoto kutoka jamii ya kifugaji ya Maasai kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi vyuo kikuu.
Inadaiwa kuwa hata baadhi ya vijana wa Kimaasai wanaoongoza mapambano ya kuipiga vita kampuni hiyo kupitia NGO walizozianzisha baada ya kuhitimu masomo, wamesomeshwa aidha kwa gharama zote za elimu yao au sehemu kulipiwa na OBC.
Kampuni hiyo imechimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali Loliondo, ingawa nakiri kutojua uhakika wa upatikanaji wa maji katika visima hivyo.
Miaka ya tisini, OBC ilitoa mabasi kwa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro ili kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa Loliondo.
Licha ya madai ya mabasi hayo kuhitaji gharama kubwa ya uendeshaji ikiwemo matumizi makubwa ya mafuta na vipuri, lakini yalipokelewa, kutumiwa na hatimaye kuwekwa juu ya mawe baada ya kampuni kuacha uendeshaji mikononi mwa halmashauri.
Nimeeleza kwa kirefu baadhi ya mambo, yaliyotendwa na OBC ili kujenga hoja ninayolenga kuijadili ambayo ni kwanini wananchi wa Loliondo wameendelea kupiga vita OBC kwa miaka zaidi ya 20 sasa.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post