Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Stephen Wasira amesema yeye ni waziri na ana haki zake, baada
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kumtaka aachie nyumba
anayoishi ya Bodi ya Sukari kwa kuwa haimuhusu kwa sasa.
Juzi, PAC iliiagiza Bodi ya Sukari Tanzania (SBT)
kumwandikia barua ya kumtaka mwanasiasa huyo mkongwe aondoke kwenye
nyumba ya bodi hiyo iliyopo Masaki jijini hapa, aliyoishi tangu akiwa
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na iwapo haitawezekana, aanze
kulipia tozo ya pango.
Hata hivyo jana, Wasira aliiambia gazeti hili kuwa
hawezi kujibizana na PAC kwa kutumia magazeti na kwamba kama kuna
maagizo yoyote yametolewa, kipo chombo kitakachoshughulikia.
“Mimi ni waziri nina haki zangu, PAC haihusiki na
mtu binafsi wala siyo ofisa mahesabu. Kwa nini unaniuliza mimi, si
uwaulize PAC?” alihoji Wasira.
Akijibu maelezo hayo ya Wasira, mwenyekiti wa PAC,
Zitto Kabwe alisema jana kuwa kamati yake haina nia ya kumshambulia
waziri huyo kwa kuwa ana haki ya kupewa nyumba na Serikali.
Alisema iwapo Serikali bado inataka waziri huyo
aendelee kukaa kwenye nyumba hiyo, ilipe kodi na kama ikishindwa wampe
nyumba nyingine.
“Hapa suala siyo mzee Wasira binafsi, ni Serikali
kukaa kwenye nyumba ya umma isiyolipia kodi,” alisema Zitto. Aliongeza
kuwa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndiyo
iliyobaini kuwa nyumba hiyo hailipiwi kodi na kuitaka irejeshwe kwa
Bodi ya Sukari.
إرسال تعليق