Dar es Salaam. Hii ni wiki ngumu kwa wenyeviti
watatu wa Kamati za Bunge ambao wanatakiwa kuachia nafasi za uongozi
kutokana na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ya Sh306
bilioni.
Wenyeviti wanaotakiwa kuvuliwa uongozi na Wajumbe
wa Kamati husika ni Andrew Chenge (Bajeti) William Ngeleja (Katiba) na
Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini).
Katika mkutano wa 16 na 17 wa Bunge liliazimia
watu walioshiriki katika kashfa hiyo wakiwamo viongozi wa kamati hizo
tatu, wachukuliwe hatua za haraka na Kamati husika za Bunge kabla ya
kuanza kwa mkutano wa 18 wa Bunge, Januari 27 mwaka huu.
Licha ya maazimio hayo ya Bunge, Kamati hizo
zimeshindwa kutekeleza uamuzi huo huku wenyeviti hao wakiendelea
kujitambulisha kuwa ni wenyeviti wa Kamati hizo jambo ambalo limekuwa
gumzo tangu kuanza kwa vikao hivyo Januari 13 mwaka huu.
Januari 15 mwaka huu, Kamati ya Nishati na Madini
iliyokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti, Jerome Bwanausi ilikutana na
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na wakati wa
kujitambulisha Mwambalaswa alijitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa kamati
hiyo.
Katika kikao kimojawapo cha Kamati ya Bajeti wiki
iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu
aliongoza na wakati kikao kikiendelea, Chenge alikuwa pembeni.
Hata hivyo, siku mbili baadaye, Chenge alisema
kuwa hakuwahi kujitangaza kujiondoa katika nafasi ya uenyekiti lakini
anashangaa kutangazwa katika vyombo vya habari.
Wiki hii pia, Ngeleja aliliambia gazeti hili
kwamba anaendelea kushikilia nafasi hiyo kwa maelezo kuwa uchunguzi wa
suala hilo bado unaendelea, ikithibitika ndipo Bunge litachukua uamuzi
ambao alidai yupo tayari kuutekeleza.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah alisema,
“Kazi ya Spika (Anne Makinda) ni kusimamia utekelezaji wa maazimio hayo
na jukumu la kuwaondoa lipo mikononi mwa kamati husika lakini hata hivyo
bado kuna muda ambao kamati hizo zinaweza kutekeleza azimio hilo.”
Akinukuu azimio hilo Dk Kashilillah alisema,
“Kamati husika za kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa
vyovyote vile kabla ya mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao
kwenye kamati husika za kudumu za Bunge.”
Aliongeza: “Sasa kwa hili mimi na Spika
tunaingiaje?, Spika yeye anasimamia utekelezaji wa maazimio hayo na kama
itashindikana atachukua uamuzi wa kuwahamisha kamati jambo ambalo
(mwenyekiti) akihamishwa anapoteza sifa ya kuwa mwenyekiti lakini kwa
sasa waulizeni wao wenyewe wanafanya lini chaguzi hizo.”
Wiki ya mwisho
إرسال تعليق