Wanafunzi 48 wasichana wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari ya
vipaji maalum ya Muungano wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro
wamenusurika kifo baada ya bweni lao kuteketea kwa moto na vifaa vyao
vyote.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo ya wananchi Mh Zawadiel Maruchu
amesema, moto huo ulianza kwenye bweni hilo kuanzia saa moja usiku
wakati wanafunzi wakijiandaa kupata chakula lakini hamna aliyejeruhiwa.
Mh Maruchu amevipongeza vyombo vya ulinzi, zima moto na wananchi
kwa ushirikiano wao mkubwa uliofanikisha kuzimwa kwa moto huo ambao
umetekeza vifaa vyote ingawa kuna mabaki kidogo ya nguo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Moshi Bw Flugence
Mponji amesema, wanafunzi wa kidato hicho wamerudishwa nyumbani kwao kwa
wiki moja wakati serikali inafanya juhudi za haraka kuwatafutia malazi.
Wanafunzi wa shule hiyo wameiomba serikali iimarishe ulinzi na
kuweka uzio wa shule na kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo
ambalo limeacha maswali mengi miongoni mwa wananchi wa kata ya kilema
kusini.
Wazazi wa wanafunzi hao wameiomba serikali iweke miundo mbinu yenye
hadhi ya shule hiyo kuwa ya bweni ya wasichana wa vipaji maalum kuliko
hali ilivyo sasa ambayo mazingira yake ni hatarishi.
إرسال تعليق