Mbinga.Watoto wanne kati ya sita wamenusurika
kifo, wilayani Mbinga, Mkoa wa Ruvuma baada ya kulipukia na kitu ambacho
kimeunganishwa na nyaya nyingi, kinachodaiwa kutumika kulipulia miamba
ambacho kimewajeruhi vibaya.
Taarifa za awali ambazo zilisambaa mjini Mbinga,
ilielezwa kuwa mlipuko huo ulitokana na kitu ambacho kilidhaniwa kuwa ni
bomu ambalo limetengenezwa kienyeji, jambo ambalo siyo kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela, alithibitisha kuwa, tukio
hilo lilitokea Januari 2, saa 5:30 asubuhi katika Mtaa wa Kiwandani
mjini Mbinga mkoani Ruvuma, wakati watoto hao wakiwa wanachezea
vilipushi hivyo walivyoviokota kwenye jalala.
Msikhela alikitaja kitu hicho kuwa ni vilipushi
ambavyo vinadaiwa kuwa vinatumika na watafiti wa madini migodini au
walipuaji baruti na akieleza kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya na
liliwakumba watoto hao baada ya kuokota kifaa hicho jalalani.
Aliwataja watoto waliolipukiwa kuwa ni Philiberth
Mbungu (10), Augustino Millanzi (5), Geofrey Ndunguru (8) na Emmanuel
Mwingira (7) ambao wote wameumizwa sehemu mbalimbali na wengine wawili
Ayubu Methew (10) na Hassan Mapangi (5) wakiwa na majeraha ya kawaida
mwilini.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Elisha Robert
alifafanua kuwa mtoto Philiberth na Augustino wamehamishiwa katika
hospitali ya mkoa iliyopo Songea kwa matibabu zaidi.
Alisema watoto hao wamepelekwa huko kutokana na
kujeruhiwa vibaya sehemu za usoni pamoja na machoni, ambapo kuna vipande
vidogo vidogo vya vyuma vimeingia ndani yake.
“Niliamua kuchukua hatua ya kuwapeleka hospitali
ya mkoa ili wakapatiwe matibabu zaidi kutokana na jinsi nilivyowaona
hali zao siyo nzuri na mimi naendelea kufuatilia kujua hali zao
zinaendelea aje huko, lakini taarifa nilizonazo mpaka sasa tayari
wamepokewa na wamehudumiwa,” alisema Robert.
Aliongeza kuwa Geofrey na Emmanuel wanaendelea
kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ambapo nao wamejeruhiwa usoni na
mikononi na hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda Msikhela alisema uchunguzi unaendelea
kuhusu tukio hilo na alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuwa
waangalifu na watoto wasiwaachie wakitembea hovyo, hivyo pale wanapoona
kitu chenye muunganiko wa nyaya wasikiguse bali watoe taarifa mapema
kwenye vyombo vya usalama ambavyo vipo karibu nao
إرسال تعليق