Ni mwafaka ramli kupigwa marufuku

Jana baadhi ya vyombo vya habari nchini, viliripoti kuwa serikali imepiga marufuku waganga wa jadi wanaotibu kwa kupiga ramli.
Vyombo hivyo vya habari vilimnukuu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, akizungumza jijini Dar es Salaam juzi.

Chikawe alisema Jeshi la Polisi na Chama cha Maalbino Tanzania (TAS), wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya operesheni ya ukaguzi kuwabaini waganga wa jadi watakaokiuka agizo hilo.

Alibainisha kuwa ili operesheni hiyo itekelezwe, wizara yake itashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kuwabaini waganga hao katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Chikawe alisema lipo wimbi kubwa la waganga wapiga ramli ambao huwadanganya watu kwamba watapata nafasi mbalimbali za madaraka ukiwamo ubunge, udiwani ama kupandishwa vyeo maofisini mwao.

Kadhalika, alisema wapiga ramli hao huwatapeli watu kwa kuwaambia kuwa wana uwezo wa kuwafanya wawe matajiri, jambo alilopinga Waziri Chikawe na kueleza kwamba kimsingi hakuna utajiri wowote wa haraka haraka pasipo kufanya kazi kwa bidii.

Ili watu hao wafanikishe hayo, Waziri Chikawe alisema wapiga ramli hao huwapa masharti wanaohitaji huduma hiyo ikiwamo kuwateka na  kuwaua albino.

Alisema kutokana na ramli hizo kuwa chanzo cha mauaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ya kuipiga marufuku.

Sisi tunaunga mkono uamuzi huu wa serikali ambao tunaamini kwamba utasaidia kurejesha amani na utulivu si kwa jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi tu, bali pia kwa vikongwe ambao huuawa kila uchao, chanzo kikiwa ni upigaji wa ramli.

Ingawa wapiga ramli wametapakaa kila kona ya nchi, lakini ni bahati mbaya sana matukio ya utekwaji na mauaji ya albino pamoja na vikongwe, yameshamiri sana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mikoa ambayo mauaji ya namna hiyo yamekithiri ni Shinyanga, Geita, Simiyu, Mwanza na Tabora.

Upigaji ramli, ni moja ya utapeli mkubwa uliojikita ndani ya jamii kwani wengi wa wapiga ramli hutoa majibu ya uchonganishi katika jamii.

Zipo sababu kadha wa kadha ambazo humfanya mtu akimbilie kwa waganga wa jadi kupiga ramli, lakini kubwa ni ukosefu wa elimu na dhana za kishirikina.

Mathalani, mtu anapofiwa ama kuuguliwa na nduguye, huamini kwamba kuna `mkono wa mtu' yaani amerogwa.

Jamii iliyotawaliwa na fikra za imani za kishirikina, daima huamini kwamba kila kifo ni cha kurogwa na hakuna kinachotokana na mapenzi ya Mungu ama maradhi yanayotokana na mazingira yetu tunayoishi.

Ni kwa msingi huo basi, ndipo mtu anapofiwa na nduguye, huamua kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli ambako hudanganywa.

Matokeo ya ramli yamethibitisha vifo vya ndugu zetu albino na vikongwe wasio na hatia.

Kwa mfano, takwimu za kuanzia mwaka 2006 zinaonyesha kuwa albino 74 wamekwisha kuuawa nchini huku 56 wakinusurika kifo na 11 kupata ulemavu mwingine wa kudumu.

Aidha, zipo taarifa kwamba takribani vikongwe 500 huuawa kila mwaka kutokana na imani za kishirikina, lakini kubwa zikichangiwa na waganga wa jadi wapiga ramli.

Na ndiyo maana tunasema hatua hii ya kupiga marufuku upigaji ramli, sasa itasaidia sana kuleta amani na utulivu ndani ya jamii.

Tunajua na kutambua umuhimu wa tiba za asili lakini hii ya kupiga ramli, tunasisitiza kwamba hapana na haina tija ndani ya jamii zaidi ya kuleta chuki na mifarakano.

Hatua hii ya kupiga marufuku ramli imepokewa kwa furaha kubwa miongoni mwa wadau kikiwamo Chama cha Albino Tanzania (TAS).

Akizungumzia uanzishwaji wa operesheni hii, Mwenyekiti wa TAS, Ernest Kimaya, aliipongeza serikali kwa kuanzisha operesheni hiyo akisema kwamba kilio cha muda mrefu cha albino kimesikilizwa.

Hata hivyo, Kimaya alivitaka vyombo vya habari na  wananchi, kutoa ushirikiano ili kuhakikisha taarifa za vitendo hivyo zinafikishwa katika vyombo vya usalama.

Ni matumaini yetu kwamba kikosi kazi hiki kitafanya kazi kwa weledi mkubwa kuhakikisha kwamba si tu jamii ya albino sasa inaishi kwa amani, bali pia hata vikongwe ambao ni hazina kubwa ya busara kwa jamii yetu.
 

CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم