Ofisa habari ajitosa ubunge Mbinga Mashariki

Mbinga. Ofisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Humphrey Kisika (32) ametangaza nia ya kuwania ubunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Ukata wilayani Mbinga juzi, Kisika alisema anataka kupokea kijiti kutoka kwa mbunge wa sasa, Gaudance Kayombo.
Alisema anautambua na kuuthamini mchango alioutoa mbunge huyo, lakini umefika muda wa yeye kupumzika na kuwaachia wengine nao wawatumikie wakazi wa jimbo hilo.
Alisema amebaini bado kuna pengo linalodumaza maendeleo kati ya wataalamu ambao ni watendaji wa shughuli mbalimbali za Serikali na wananchi ambao ni wapigakura.
“Kuna manung’uniko mengi kutoka kwa wananchi yanayochangiwa na baadhi ya watendaji ambao kwa masilahi yao binafsi au kwa sababu ya kufanya kazi kwa mazoea, wanashindwa kuutumikia vyema umma wa Watanzania,” alisema.
Kisiki, ambaye anataka kujaribu bahati yake kwa kupitia CCM, alisema chama hicho kina sera nzuri zinazoshindwa kufanya kazi kutokana na uzembe wa baadhi ya watendaji.
Akizungumzia mwonekano wa kundi kubwa la vijana kushabikia zaidi vyama vya upinzani, alisema katika mazingira ambayo nchi inaendeshwa kwa misingi ya demokrasia kama Tanzania, hali hiyo lazima itajitokeza.
Hata hivyo, alisema hiyo haimaanishi kuwa vijana wote ni wafuasi wa vyama vya upinzani.
“Ombi langu kwa vijana wenzangu, ni muhimu katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa tukafanya siasa kwa misingi ya upendo na amani, tusikubali kutumiwa kwenye harakati za siasa chafu zitakazohatarisha amani ya nchi hii, tunataka iendelee kuwa kisiwa cha amani,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post