PAC yabaini upotevu wa fedha zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 mamlaka ya Bandari TPA.

Kamati ya bunge ya hesabu za serikali PAC imebaini upotevu wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA ambazo zimetumika lakini nyaraka zake hazionekani huku ikiuagiza uongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha fedha zote za nyongeza ya posho za safari walizolipwa watumishi tangu mwaka 2011 kabla msajili wa hazina hajathibitisha zinarudishwa.
Mwenyekiti wa kamati ya PAC Mh Zitto Kabwe ametoa agizo hilo wakati kamati yake ilipokutana na bodi na uongozi wa TPA baada ya kukagua vitabu vyake vya mahesabu ambapo amesema licha ya kiwango cha posho zilizolipwa kuwa kikubwa lakini waliharakisha kujilipa kabla msajili wa hazina hajathibitisha ambapo afisa wa ngazi ya juu alilipwa shilingi laki tano kwa siku kwa safari ya ndani ya nchi na ya nje ya nchi dola za kimarekani mia nane.
Akizungumzia suala la ukosefu wa nyaraka za fedha ambazo tayari zimeshatumika makamu mwenyekiti wa PAS Mh.Deo Philikonjombe amesema tatizo hilo limekuwa sugu kwa taasisi mbalimbali za serikali hali inayoashiria kuwa kuna baadhi ya wakurugenzi na watumishi wanafuja fedha za umma kinyume na taratibu na wanapobanwa wanapeleka nyaraka ambazo wakati mwingine ni za kufoji.
Kaimu mkurugenzi mkuu wa TPA na mhasibu wake mbali na kukiri upotevu wa nyaraka hizo wamedai kuwa tatizo hilo limetokana na uhifadhi wa nyaraka ambao hadi leo nyaraka nyingi za TPA zinahifadhiwa kwenye karatasi na kuiahidi kamati hiyo kuwa wataziwasilisha mwisho wa mwezi wa mwezi febuari mwaka huu hali iliyozua maswali mengi kwa wajumbe wa kamati hiyo kuwa watazipata wapi kama kipindi chote hicho hazijaonekana.

Post a Comment

أحدث أقدم